BANDA MEDIA BLOG

MBETO: ALICHOKIPATA DKT. NCHIMBI KINAMSTAHIKI

 

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Komredi Khamis Mbeto Khamis, amesema hatua zilizochukuliwa dhidi ya Dkt. Emmanuel Nchimbi,aliekua Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinamstahiki kutokana na kile alichodai kuwa ni dharau na kiburi dhidi ya chama hicho na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mbeto aliyasema hayo Agosti 28, 2026, wakati akizungumza na wanahabari katika Ofisi za CCM Kisiwandui, mjini Unguja, ambapo alisema Dkt. Nchimbi aliitwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM Taifa chini ya mwenyekiti wake Mzee Steven Wassira, kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusu kauli alizokuwa akizitoa, lakini hakutokea.

Alisema licha ya kuitwa Dodoma, Dkt. Nchimbi hakufika katika kikao hicho, akisisitiza kuwa hakukuwa na sababu ya msingi iliyomzuia kuhudhuria.

“Hakuwa nje ya nchi wala hakuwa na changamoto yoyote ya kumfanya asiende Dodoma,” alisema Mbeto.

Alieleza kuwa baada ya Dkt. Nchimbi kutofika Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mzee Steven Wassira, aliona umuhimu wa kumfuata Dar es Salaam ili kumpa nafasi nyingine ya kutoa ufafanuzi.

Mbeto alisema Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alitoa ndege kwa ajili ya wajumbe wa kamati hiyo, ingawa hatua hiyo haikuwa sehemu ya utaratibu wa kawaida, ili waweze kwenda Dar es Salaam na kukutana na Dkt. Nchimbi katika eneo ambalo lingefaa.

Hata hivyo, alisema Dkt. Nchimbi hakutokea tena katika kikao hicho.

“Dkt. Nchimbi alipewa nafasi, lakini kwa masikitiko makubwa hakuitumia. Badala yake ameonyesha jeuri, kutoa visingizio visivyo na sababu na kukaidi wito huo,” alisema.

Mbeto alisema hatua hiyo ilikuja licha ya uungwana ulioonyeshwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisema alikuwa amemwamini Dkt. Nchimbi na hata kumpendekeza kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu uliopita.

Alisema katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika Ikulu Ndogo Tunguu, Julai 29, 2026, tuhuma zinazohusiana na kauli za Dkt. Nchimbi ziliwasilishwa na Kamati Ndogo ya Maadili na Usalama ya CCM Taifa, ambayo iliagizwa kumuita ili athibitishe au kutoa ufafanuzi kuhusu kauli hizo.

“Pamoja na yote, CCM chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Samia, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitumia uungwana na kusisitiza aitwe kwenye Kamati Ndogo ya Maadili na Usalama ili asikilizwe katika kile ambacho kinaitwa tuhuma dhidi yake,” alisema.

Mbeto alisisitiza kuwa hatua iliyochukuliwa dhidi ya Dkt. Nchimbi inastahiki, akidai kuwa mwenendo wake ulionesha kutokuwa na nia njema na chama pamoja na kuonyesha jeuri na dharau kwa uongozi wa CCM.

Alisema CCM ni chama kikubwa kuliko mtu na kwamba katika kikao cha Tunguu mambo mbalimbali yaliibuka, baadhi yake yakiwa hayafahamiki hata kwa baadhi ya wajumbe.

Mbeto alisema kwa mujibu wa taratibu za chama, usaliti ni miongoni mwa makosa yanayoweza kusababisha mwanachama kufukuzwa, akisema hatua hiyo ndiyo iliyotekelezwa dhidi ya Dkt. Nchimbi.

AMpongeza NDEJEMBI

Katika hatua nyingine, Mbeto amempongeza Makamu wa Rais Mteule, Deogratias Ndejembi, akisema CCM imemchagua kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba kwa mujibu wa Katiba, uteuzi huo unasubiri kuidhinishwa na Bunge.

Mbeto alisema anamfahamu Ndejembi kwa muda mrefu, baada ya kuwa pamoja katika Baraza la Taifa la Chama (NEC) mwaka 2012, na kumuelezea kuwa ni mchapakazi ambaye ameendelea kuonyesha uwezo katika nafasi mbalimbali alizowahi kushika.

“Ndejembi nilikuwa naye mjumbe wa NEC mwaka 2012. Ni mchapakazi na ameonyesha ubora katika kila nafasi anayoteuliwa au kuchaguliwa,” alisema Mbeto.

Aliongeza kuwa uzinduzi wa Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere uliofanyika hivi karibuni ni miongoni mwa matukio yanayoonyesha namna Ndejembi anavyowajibika na kujituma katika utekelezaji wa majukumu yake.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG