BANDA MEDIA BLOG

MZEE WA MIAKA 85 AMLALAMIKIA MWANAWE KUDAI NYUMBA YAKE KWA NGUVU,RC SENDIGA AINGILIA KATI

 Na John Walter -Babati

Mzee Juma Boki (85), mkazi wa Babati mkoani Manyara, amemlalamikia mwanawe, Salimu Boki, kwa madai ya kujimilikisha nyumba yake iliyopo eneo la Osterbay, Babati, huku akidai amechukua hati ya nyumba hiyo na kuanza kukusanya kodi kutoka kwa wapangaji bila ridhaa yake.

Akizungumza baada ya kutembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, mzee huyo alisema Salimu amekuwa akisisitiza kuwa nyumba hiyo ni mali yake akidai kuwa aliandikishwa kuirithi alipokuwa na umri wa miaka mitano, na baadaye alikabidhiwa nyaraka za umiliki alipofikia utu uzima.

Hata hivyo, Mzee Boki alisema nyumba hiyo ni mali yake na kwamba amesikitishwa na hatua ya mwanawe kuchukua hati ya nyumba pamoja na kutomjali licha ya kuwa anaumwa.

“Kwa sasa ameweka wapangaji kwenye nyumba hizo na ndiye anayechukua kodi. Mimi ni mgonjwa lakini hata kunijulia hali hawaji,” alisema mzee huyo ambaye ana wake wawili na jumla ya watoto 12.

Kutokana na hali hiyo, Mzee Boki aliwasilisha barua ya malalamiko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara akiomba msaada wa serikali ili apate haki yake.

Baada ya kupokea malalamiko hayo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alimtembelea mzee huyo nyumbani kwa binti yake katika mtaa wa Nyunguu, ambapo alimkabidhi zawadi mbalimbali zikiwemo sukari na mahitaji mengine, huku akitaka kufahamu kwa undani mgogoro huo.

Akiwa ameambatana na baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Sendiga alimhoji Salimu Boki kuhusu madai yanayomkabili.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika kikao hicho, Salimu alikana madai hayo na kueleza kuwa hafahamu kuhusu kesi inayozungumziwa, akisisitiza kuwa nyumba hiyo ni mali yake.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo kwa vyombo vya dola kumshikilia Salimu Boki kwa mahojiano zaidi, huku akisema ataendelea kufuatilia suala hilo hadi litakapopata ufumbuzi kwa mujibu wa sheria.

Mhe. Sendiga pia aliahidi kuhakikisha haki inatendeka kwa kufuata taratibu na sheria za nchi ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya haki.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG