Askofu Jacob William Kahemele wa Dayosisi ya Southern Highlands, ameongoza Misa ya Maadhimisho ya Msalaba Mtakatifu iliyofanyika katika Mtaa wa Msalaba Mtakatifu, Nambunga – Dayosisi ya Newala, iliyofanyika Septemba 13, 2026.
Askofu Kahemele ameeleza kwa kina historia ya Msalaba Mtakatifu, maana yake katika imani ya Kikristo, pamoja na umuhimu wake kwa waamini katika maisha ya leo. Amewakumbusha waamini kwamba Msalaba ni ishara kuu ya kazi ya Kristo ya ukombozi na msingi wa tumaini la Mkristo.
Katika ziara hiyo, Askofu Kahemele pia amewapongeza waumini wa Mtaa wa Msalaba Mtakatifu Nambunga kwa jitihada zao katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, akiwataka kuendelea kushirikiana katika kuijenga na kuiimarisha kazi ya Mungu.
Aidha, amewashauri waumini kuwa mabalozi wema wa kulinda na kutetea mipaka ya maeneo ya Kanisa, hususan ardhi ya Kanisa, kwa kuzingatia taratibu na sheria, ili kuepuka changamoto za uvamizi na migogoro ya ardhi.
Askofu Kahemele pia amesisitiza dhamira yake ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano mema kati ya Dayosisi ya Southern Highlands, Mtaa wa Msalaba Mtakatifu Nambunga na Dayosisi ya Newala kwa ujumla, akieleza kuwa ushirika na umoja wa Kanisa ni muhimu katika kuendeleza utume wa Kristo.
Akizungumza kwa niaba ya waumini wa Msalaba Mtakatifu Nambunga, Lay Canon Kapteni Mstaafu George Huruma Mkuchika amemshukuru Askofu Kahemele kwa upendo wake na kwa kufika Nambunga kuungana nao na kuongoza Misa ya maadhimisho hayo.
Lay Canon Mkuchika pia ametoa wito kwa Kanisa kuendelea kujenga uwezo wa kiuchumi na kujitegemea katika utekelezaji wa shughuli za utume, badala ya kutegemea kwa kiasi kikubwa wafadhili kutoka nje.
Maadhimisho hayo yamekuwa sehemu ya kuimarisha imani, ushirika na mshikamano wa Kanisa, huku waamini wakikumbushwa kwamba Msalaba wa Kristo unaendelea kuwa alama ya upendo, wokovu na tumaini kwa ulimwengu.












