BANDA MEDIA BLOG

Futeni madeni yao, watumeni kuivamia Iran: Gazeti la Israel lapendekeza mpango kwa Wamarekani

Jerusalem Post inahoji kuwa Marekani inaweza kuajiri mamilioni ya vijana wenye madeni kwa ajili ya vita vya ardhini dhidi ya Iran. / TRT World / TRT World

...............

 Makala iliyochapishwa katika gazeti la Israel imependekeza kuwa Marekani inapaswa kufuta madeni ya vijana wa Marekani iwapo watakubali kujiunga na uvamizi wa Iran; mwandishi anahoji kuwa vita vya Marekani dhidi ya Iran haviwezi kushindwa kwa mashambulizi ya anga pekee, bali vingehitaji kuikalia au kuidhibiti nchi hiyo, jambo linalohitaji kuhamasisha na kupeleka hadi askari milioni 1.5.


Pendekezo hilo la kushangaza la kuwatumia vijana wa Marekani wenye madeni kama chambo cha vita (watu wa kutolewa kafara) dhidi ya Iran lilitolewa na AJ Jaff, afisa mstaafu wa Jeshi la Canada, katika makala ya maoni iliyochapishwa na gazeti la Jerusalem Post.

Katika hoja zake, Jaff anasema kuwa miezi kadhaa ya mashambulizi makali ya Marekani haikuweza kusambaratisha uwezo wa kijeshi wa Iran wala kumaliza vita, na kwamba uvamizi wa nchi kavu ungehitaji askari wengi zaidi wa Marekani kuliko idadi iliyopo sasa.

"Idadi ya watu wanaojiunga na jeshi iko chini ya kiwango kinachohitajika kwa uvamizi wa nchi kavu dhidi ya Iran. Makadirio ya operesheni ya nchi kavu yenye mafanikio dhidi ya vitengo vya kijeshi vya mikoa 31 ya Iran na 'Mafundisho yake ya Ulinzi ya Mosaic' (Mosaic Defense Doctrine) yanaonyesha hitaji la askari wa Marekani kati ya 750,000 na milioni 1.5. Kwa sasa, Jeshi la Marekani lina askari hai wapatao 452,000. Ni wazi kuwa hesabu hizo hazilingani," anaandika mwandishi huyo.

Jaff anahoji kuwa historia ya Marekani inaonyesha njia mwafaka ya kusonga mbele: kuajiri askari kupitia mpango wa kufuta madeni badala ya mfumo wa kawaida wa kulazimisha watu kujiunga na jeshi wakati wa vita.

"Mmarekani wa kawaida mwenye umri wa miaka 18 hadi 34 ana mzigo wa deni la zaidi ya dola 40,000—bila kujumuisha mikopo ya nyumba—likijumuisha mikopo ya elimu ya juu, madeni ya kadi za mkopo, mikopo ya magari, na mikopo binafsi; huku makadirio mengine yakionyesha deni hilo linaweza kufikia hadi dola 100,000," anaandika, akiongeza kuwa hii ndiyo kundi la watu ambalo Pentagon inalihitaji.

"Mpango wa kujiunga na jeshi unaosimamiwa na serikali kuu, ambao unafuta kabisa mikopo ya elimu ya juu, madeni ya kadi za mkopo, na salio la mikopo mingine baada ya miezi 24 au 36 ya utumishi, na pia kupanua wigo wa 'GI Bill' (mpango wa marupurupu kwa wanajeshi), ungesababisha watu wengi kujiunga na jeshi kwa hiari," anahoji mwandishi huyo.

Pendekezo lisilo la kawaida

Takriban asilimia 77 ya Wamarekani wana aina fulani ya deni. Hii inamaanisha kuwa takriban watu milioni 250 hadi 260 wanakabiliwa na aina mbalimbali za madeni, jambo linalochangia jumla ya kihistoria ya deni la kil anyumba nchini Marekani kufikia dola trilioni 18.8. Kwa wastani, watu wazima nchini Marekani walikuwa na deni la dola 63,500.

Jaff anataja mifano ya awali nchini Marekani kuhusiana na mipango kama hiyo ya kuajiri watu jeshini, akibainisha kuwa Vita vya Pili vya Dunia vilileta mpango wa 'GI Bill', huku Vita vya Vietnam vikitoa fursa ya kuahirishwa kwa masomo ya chuo kikuu.

"Vita vilivyofuata shambulio la 9/11 vilitoa bonasi za kujiunga na njia za kupata uraia. Vita dhidi ya Iran vitahitaji kutoa unafuu wa madeni. Hali ya kiuchumi ya Wamarekani wenye umri wa kati ya miaka 20 na 30 walio na madeni inafanya hili kuwa njia bora zaidi ya kuwavutia watu kujiunga na jeshi inayopatikana kwa Pentagon na utawala wa Trump," mwandishi anasisitiza.

Anaelezea mpango huo kama jambo lisilokubalika kimaadili lakini pia anauita "njia bora zaidi ya kuwavutia watu kujiunga na jeshi" kwa Pentagon na utawala wa Trump, akisema kuwa nchi huajiri watu kwa kuandaa vivutio vinavyolingana na makundi mahususi ya watu wake.

Makala ya Jaff iliwasilisha mpango huo wa kutisha kama mojawapo ya njia tatu zisizohusisha mapigano ya moja kwa moja (non-kinetic options) ambazo Washington inaweza kutumia kuishinda Iran, sambamba na hatua ya Bunge la Marekani kutambua uhuru wa makundi madogo ya watu nchini Iran na makubaliano na China kuhusu mafuta ya Iran.

Makala hiyo imezua ukosoaji mkubwa; wengi wakitupilia mbali mapendekezo hayo wakiona yana kasoro kwa mtazamo wa Marekani, wengine wakihoji uwezo wa mwandishi, na baadhi wakidai kuwa Israel inataka kupigana na Iran "hadi Mmarekani wa mwisho".

Vyombo vya habari kama vile The Blaze vilielezea pendekezo hilo kama unyonyaji usiofaa au wa hila wa hali ya Wamarekani kuwa na madeni. Kilielezea mpango wa Jaff kama pendekezo lisilo la kawaida la kuwapeleka mstari wa mbele vijana wa Marekani waliolemewa na madeni.

Taasisi ya Mises ilipa makala yake kichwa cha habari 'The Jerusalem Post Yataka Wamarekani Zaidi Kujiunga na Jeshi – ili Wafe kwa Ajili ya Israel', ikielezea makala hiyo kama ujumbe kutoka chombo cha habari cha Israel unaowataka walipa kodi wa Marekani kufadhili vita vingine.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG