MTANDAO wa wafanyabiashara wa bidhaa za majimaji na zile zinazotengenezwa katika mazingira yasiyo salama wazidi kuutesa uongozi wa baraza la Mji Wete , baada ya kuibuka na mbinu mpya ya kuendesha biashara zao .
Mbinu zilizoibuliwa na wafanyabiashara zao ni kuuza bishaa zao wakati wa jioni baada ya muda wa kazi kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Serikali ikiwemo baraza la Mji kufunga ofisi na hushamiri zaidi nyakati za usiku .
Biashara hizo zimepigwa marufku kuendelea kutumika katika Mji huo baada ya kuzuka mripuko wa magonjwa ya matumbo ikiwemo kipindupindu na kuharisha katika baadhi ya maeneo ya Mji wa Wete .
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wete Mgeni Othman Juma amekiri kwamba kitendo hicho na kuwashauri wananchi kuheshimu tamko la Serikali ili kunusuru kukumbwa na ugonjwa wa Kipindupindu .
Amesema kwamba pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Uongozi wa baraza kudhibiti biashara hizo , lakini zinakwamishwa na wachache ambao wanatamaa ya fedha bila ya kujali madhara yanayoweza kutokea siku za baadaye .
“Lengo la kupiga marufuku biashara hizo ni kuzuia kuendelea kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu , lakini baadhi ya wafabiashara wameshindwa kuheshimu agizo na hivyo kuendelea kuuza wakati wa jioni na nyakati za usiku ”alifahamisha .
Akizungumzia suala la elimu kwa wafanyabiashara juu ya kufunga biashara zao , alisema kwamba tayari uongozi wa baraza umepita katika kila mitaa na kona za Mji huo baada ya kutokea kwa mripuko wa Ugonjwa wa kipindupindu na kuwataka wasimamishe shughuli zao kwa muda .
Alifahamisha kwamba kazi hiyo aliifanya kwa ushirikiano mkubwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo baadhi ya wananchi walionekana kutoa maneno ya kejeli wakati zoezi hilo la kuwaelimisha wananchi kutambua njia za zinazoeneza ugonjwa huo .
“Tulipata maneno ya kejeli lakini tulivumilia na kutumia hekima ya uongozi , tulitambua kwamba itafikia wakati watafahamu na hivyo kutii agizo , lakini cha kushangaza baadhi ya wananchi walisikika wakisema tunasumbuliwa na njaa ”alieleza .
Naye Mlenge akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba , alisema kwamba , jeshi hilo liko tayari kushirikiana na uongozi wa Baraza kufanya operesheni ya kuwasaka wafanyabiashara wanaokiuka agizo la Serikali .
“Hata sasa iwapo Uongozi wa Baraza utakuwa tayari kufanya operesheni , askari wako tayari kuongoza kamatakamata hiyo wakati wowote iwe mchana ama usiku ”alisisitiza Mlenge .
Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya kupigwa marufuku kwa biashara hizo , walisema kwamba kitendo hicho kimelenga kudhoofisha shughuli zao za kupambana na umaskini .
Walisema kwamba Serikali inapaswa kujali na kuthamini juhudi za wafanyabiashara wadogo wadogo kama wauza juisi , mchungwa , uji pamoja na bidhaa nyingine ili waweze kukabiliana na ukali wa maisha .
“Ni kweli tangazo la kuzuia uuzaji wa biashara za majimajia lilitangazwa na Uongozi wa Baraza kwa kutumia mabomba na kila mmoja alilisikia , lakini tangazo hili limelenga kudhoofisha harakati zetu za kujikomboa na umaskini ”alifahamisha mmoja wa wafanyabiashara .
Serikali kupitia Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kaskazini Pemba ilifikia uwamuzi wa kuzuia uuzaji wa biashara hizo kwa muda hadi pale ugonjwa wa kipindupindu utakapomalizika na biashara hizo zitaendelea kama kawaida .
Tags
HABARI KITAIFA