Na Raymond Mushumbusi- MAELEZO
Kipindupindu ni ugonjwa wa
kuharisha na kutapika unaosababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoitwa
kwa lugha ya kitaalam “vibro cholera”. Chanzo cha kikubwa cha ugonjwa
huu huletwa na vimelea vilivyomo kwenye kinyesi na matapishi ya mgonjwa
wa kipindupindu.
Kwa miaka mingi sasa wananchi wa
Tanzania tumekumbwa na magonjwa ya aina mbalimbali ya mlipuko ukiwemo
ugonjwa wa kipindupindu ambao umeenea kwa kasi kubwa sana kutokana na
kuwepo kwa mazingira hatarishi yanayochochea mlipuko wa ugonjwa huo.
Kwa mwaka 2015 ugonjwa wa
kipindupindu umetikisa nchi yetu kwa kiasi kikubwa na kusababisha watu
kupoteza uhai na kupunguza nguvu kazi, watoto kuwa yatima wake kwa
waumwe kuwa wajane na wengine kuwapoteza ndugu jamaa na marafiki zao.
Siyo mara ya kwanza kutokea kwa
mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini ila imekuwa ni tabia ya
watanzania kuchukulia mazoea na kuuona ugonjwa huu kama michezo ya
watoto kwenye televisheni ( TV Game) na huku miaka nenda rudi
unazidi kuteketeza watanzania. kwanini watanzania hatulioni hili kuwa ni
janga la kitaifa?
Ugonjwa wa kipindupindu ulioanza
Agosti 15 2015 katika mkoa wa Dar es salaa na kuenea kwa kasi katika
mikoa mingine 20 nchini, kwa mujibu wa taarifa ya tarehe 15 Desemba 2015
kumekuwa na wagonjwa wapya 141 na kufanya jumla ya wagonjwa waliokwa
wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika
mikoa yote iliyoathirika kuwa 184 na vifo vipya viwili.
Tangu ugonjwa huu uanze jumla ya
watu 11,257 walipata ugonjwa huu na kati yao 177 wamefariki kwa ugonjwa
huu ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ya waliougua, mpaka sasa kwa wastani
ugonjwa huu umepungua katika mikoa ya Dar es salaamna kwa mkoa wa Iringa
na mji wa Moshi kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu.
Katika tamko la Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto Mhe Ummy Mwalimua alilolitoa
tarehe 16 Desemba 2015 kuhusu mapambano ya ugonjwa wa kipindupindu,
Waziri huyo alipiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyokatwa na vyakula
sehemu za wazi(barabarani) na kutoa amri watakaokiuka wachukuliwe hatua
mara moja.
“ Nahitaji nipatate taarifa ya
utekelezaji kila siku kutoka kwa Waganga wa Mikoa na Wilaya na Serikali
haitasita kuchukua hatua kwa viongozi ambao watashindwa kudhibiti
ugonjwa huu katika maeneo yao” alisema Waziri Ummy katika tamko lake
kupitia Vyombo vya Habari.
Mara baada ya kutolewa kwa tamko
hilo siku tatu baadae mwandishi wa makala hii nilifanya ziara ndogo
kuzunguka baadhi ya maeneo ya Jiji la Dares salaam hasa katikati ya Jiji
na kugundua kuwa bado kuna uuzaji wa matunda yaliyokatwa na vyakula
sehemu za wazi(barabarani) unaendelea. Katika kufatilia hilo kujua nini
Jijini limefanya hasa Manispaa ya Ilala ambayo ndo muhusika wa maeneo ya
katikati ya Jiji niliwasiliana na msemaji wa Manispaa ya Ilala Bw. Daud
Langa na kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
Msemaji wa Manispaaa ya Ilala
alisema katika suala hili watendaji wa kata na mitaa wanahusika moja kwa
moja kusimamia na kufatilia kwa karibu operesheni hii na kusisitiza
sheria za afya kuzingatiwa na hakutokuwa na huruma kwa yoyote
atakayevunja sheria.
“ Kwa mfanyabiashara yoyote
tutakayemkamata anauza matunda yaliyokatwa na vyakula maeneo ya wazi
tutamkamata na kumfungulia mashtaka ya kuvunja sheria za Afya na adhabu
yake ni faini ya Sh 30,000 au kwenda jela miezi mitatu au vyote kwa
pamoja” alisema Langa alipokuwa akitoa maelezo hayo.
Nakumbuka Desemba 9 mwaka huu
ilitangazwa kuwa ni siku ya Uhuru na Kazi na Mhe Rais Dkt Jhn Pombe
Joseph Magufuli na kuamuriwa iwe siku ya kufanya usafi katika maeneo
yetu ikiwa ni mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu ulioenea kwa
kasi . katika ziara yangu nilipita maeneo ya kawe sokoni na mto Mbezi
ambapo wananchi kushirikiana na watumishi wa taasisi za umma na binafsi
walijitokeza kufanya usafi katika maeneo hayo.
Katika maeneo ya Kata ya kawe
eneo la mto Mbezi watumishi wa iliyokuwa Wizara ya kazi na Ajira ambayo
imehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na kuwa Sera, Kazi, Ajira, Vijana na
Walemavu walijitokeza kufanya usafi wakishirikiana na wanachi wa maeneo
hayo. Cha kushangaza ni pale watumishi hao walipofika na kuanza kufanya
usafi na huku wananchi wa pale wakiwaangalia kama wafanya maonesho ya
sanaa za maigizo.
Hivi tunasubiri waje watu toka
nje ya Tanzania watusafishie maeneo yetu sisemi watanzania wote ni
wavivu hapana ndio wapo wachache waliobarikiwa kwa kuelewa nini wajibu
wao katika jamii inayowazunguka lakini wachache pia wanaharibu sifa ya
watanzania na kufanya watanzania tuonekane wavivu kazi kutoa lawama hata
kwa yale tutanayoweza kuyafanya yaliyo ndani ya uwezo wetu.
Tabia yetu watanzania tulio wengi
ni kutupia lawama na malalamiko kwa Serikali hivi kwani Serikali ni
nani? Serikali ni mimi na wewe na yule swala sio Serikali imekufanyia
nini ila wewe umeifanyia nini nchi yako? Suala la usafi liko chini ya
uwezo wetu tulifanye basi kwa bidii na hatuifanyii serikali bali
tunaifanyia nchi yetu na vizazi vyetu tukiwa na tabia ya usafi toka
tunakoishi mitaani basi itakuwa tabia ya taifa zima kwa ujumla.
Watanzania tujilaumu wenyewe
kuugua kipindupindu kwasababu tunaweza kukizuia kwa kuzingatia usafi wa
mazingira na usafi wa mipango miji pia kutojenga kwenye mikindo ya maji
mito na maziwa na vyanzo vya maji kwani maji ndo chanzo kikubwa cha
kipindupindu kwani maji yanatumika kwa asilimia kubwa katika matumizi ya
binadamu ya kila siku.
Serikali kwa upande wake
inapambana sana na suala hili la kipindupindu kwa kasi kubwa kupitia
wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto ikishirikiana
na Halmasahuri za Wilaya, Ofisi za Afya za Mikoa na Wilaya na katika
kukabilana na ugonjwa huu sekta zote husika zikiwemo Maji, Elimu,
Mawasilano, Uchukuzi na Ujenzi hazina budi kushirikiana kwa pamoja ili
kutokomeza ugonjwa huu.
Aidha wadau wa maendeleo ya
jamii hawakuwa nyuma kusaidia kampeni hii ya kutokomeza kipindupindu
nchini, mashirika kama vile shirika la Afya Duniani (WHO), CDC, USAID,
MSF, Red Cross na UNICEF kwa kushiriki katika kukabiliana na mlipuko
huu. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
wadau hawa wamechangia msaada wa fedha na vifaa vyenye thamani ya Tsh
1,884,000,000 na serikali ikatoa Tsh 900,000,000 katika kupambana na
ugonjwa huu.
Watanzania tunahamasishwa
kupambana na ugonjwa huu kwa kuona kuwa kipindupindu ni aibu kwetu mtu
kuugua ugonjwa huu wakati unazuilika kwa kuzingatia usafi tu. Wote kwa
pamoja kupitia magazeti Radio, Televisheni mitandao ya Jamii kama
Whatsaap, Twitter na Instagram tuelimishane kuhusu usafi wa mazingira
ili kutokomeza kpindupindu na kikwa historia nchini.
Kwa taarifa kuhusu ugonjwa wa
kindupindu unaweza kuzipata kupitia ujumbe mfupi kwenye simu yako
kuandika neon kipindupindu kwenda 15774 na utapata taarifa sahihi juu ya
ugonjwa wa kipindupindu na ujembe huu unapatikana bila malipo.
Tukumbuke kuwa kinga ni bora kuliko tiba, kuugua Kipindupindu ni aibu.
Tags
AFYA