|
Muonekano wa Bwawa la Mtera kwa hivi sasa ikionesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa kina cha maji.
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ametembelea Kituo cha
Kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji cha Mtera kwa lengo la kujionea hali
halisi ya kituo hicho. Akielezea hali halisi aliyoiona kituoni
hapo, Profesa Muhongo alisema kwa wakati huu kituo hicho cha Mtera
hakizalishi umeme wa kiasi chochote huku akitaja sababu kuwa ni upungufu
wa maji uliosababishwa na matumizi mabaya ya maji ya Bwawa hilo.
Profesa Muhongo alisema njia bora ya utatuzi wa upungufu wa maji kwenye
bwawa hilo la Mtera ambalo hutumiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Shirika
la Umeme Nchini (Tanesco) kwa ajili ya kuzalisha umeme ni wadau kukaa
pamoja na kukubaliana namna ya kutumia maji hayo. Mbali na
hilo, Profesa Muhongo alitaja utatuzi mwingine kuwa ni kuongeza vyanzo
vingine vingi vya kuzalisha umeme mbali na kutegemea maji ili kuruhusu
mabwawa hayo kufikia kina kinachohitajika.
|