Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi
wa Ligi umeipa Polisi Dodoma ushindi wa pointi tatu na mabao matatu
baada ya Mji Mkuu FC kumchezesha mchezaji Peter Ngowi aliyekuwa na kadi
tatu za njano kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes
iliyochezwa Desemba 26, 2015 mjini Dodoma.
Uamuzi huo umefanywa kwa
kuzingatia Kanuni ya 37(4) na 14(37) ya Ligi Daraja la Kwanza. Mji Mkuu
FC ilikuwa imeshinda mabao 2-1 katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye
Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa.
Kamishna wa mechi ya Ligi ya
Daraja la Kwanza ya StarTimes kati ya Polisi Tabora na Panone FC ya
Moshi, Shabani Funyenge amesimamishwa kutokana na ripoti yake ya mechi
hiyo iliyochezwa Januari 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora kuwa na upungufu.
Klabu ya Friends Rangers ya Dar
es Salaam imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kutokana na
washabiki wa timu yake kutoa kashfa na lugha za matusi wakati wa mechi
ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes dhidi ya Kiluvya United
iliyofanyika Novemba 8, 2015 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Kaume jijini
Dar es Salaam.
Pia imetakiwa kulipa kibendera
cha kona (corner flag) pamoja ubao wa matangazo wa geti la kuingilia
ndani kwenye Uwanja wa Karume ambavyo vilivunjwa na washabiki wa timu
hiyo mara baada ya mechi hiyo.
Mtunza vifaa wa timu ya Kimondo,
Emily Nehemia, Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Idd Kibwana, Kiongozi wa
Panone FC, Said watafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa
nidhamu kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes.
Mji Mkuu FC imepigwa faini ya sh.
100,000 (laki moja) kwa kutohudhuria kikao cha awali cha maandalizi ya
mechi (pre match meeting) katika mchezo kati yao na Polisi Dar es Salaam
uliochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Adhabu hiyo
imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
Klabu za Polisi Tabora na Panone
FC kila moja imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa mujibu
wa Kanuni ya 14(48) kugombania kuingia uwanjani kupitia mlango wa VIP
badala ya ule wa kawaida kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya
StarTimes iliyochezwa Januari 2, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi
mjini Tabora.
Wachezaji Ally Mwanyiro wa Rhino
Rangers na Hamisi Shaban wa Lipuli wamepigwa faini ya sh. 300,000 (laki
tatu) kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kupiga wachezaji wa
timu pinzani wakati wa mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes
kinyume na Kanuni ya 37(3) ya Ligi hiyo.
Pia Polisi Mara imepigwa faini ya
sh. 500,000 (laki tano) baada ya mshabiki wao kuingia uwanjani na
kumvamia mwamuzi kwa madai maamuzi yake hayakuwa sahihi wakati wa mechi
yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes dhidi ya Mbao FC iliyofanyika
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Tags
MICHEZO KITAIFA