Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Ilemela, Angelina Mabula ametoa wito kwa wakazi wa
jiji la Mwanza na maeneo ya karibu kujitokeza kwa wingi kwa sababu ya
unyeti wa Tamasha la Pasaka linalotarajia kufanyika Machi 27 kwenye
uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Akizungumza jana, Mabula alisema Tamasha la Pasaka ni la
Watanzania wote, lakini mwaka huu wamepata bahati ya kufikiwa na ujumbe
wa neno la Mungu ambao utakemea maovu kama mauaji ya vikongwe na
walemavu wa ngozi ‘albino’.
“Binaadam anatakiwa kubaki na heshima yake, kwani hakuna
maisha bora ambayo yanatokana na kuwaua na kuwakata viungo wenzao, si
ubinaadam kabisa tunatakiwa tumrudie Mungu kwani ndio kimbilio,” alisema
Mabula.
Mabula alisema Tamasha la Pasaka limebeba ujumbe wa neno la
Mungu hivyo ni nafasi kwa wakazi wa Ilemela na maeneo ya jirani na hata
mikoa mingine kujitokeza kwa wingi kufanikisha tamasha hilo.
Aidha Mabula alisema thamani ya Tamasha la Pasaka ni kubwa
hivyo Watanzania ni nafasi yetu Watanzania kumfikishia Mungu sala zetu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka,
Alex Msama alisema maandalizi ya kuelekea tamasha hilo yanaendelea
vizuri, hivyo wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wakae mkao wa kula.
Msama alisema Tamasha la Pasaka litaanza Machi 26 mkoani
Geita na kufuatiwa jijini Mwanza Machi 27 na kumalizia Machi 28 mjini
Kahama kwenye uwanja wa Taifa mkoani Shinyanga.
Msama alitaja viingilio katika
tamasha hilo ni shilingi 5000 kwa wakubwa na watoto shilingi 2000, naye
alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi
kuimuimbia na kumtukuza Mungu.