Na Athumani Adam
Kwa hakika Chelsea tayari wametupwa nje ya michuano ya UEFA Champion League msimu huu. Hiyo ni baada ya wao kupoteza tena kwenye mechi ya pili raundi ya 16 bora dhidi PSG jana usiku. Ilikuwa mechi nzuri na ushindani ambayo Chelsea walihitaji ushindi wa goli 1-0 ili kufuzu hatua ya robo fainali kitu ambacho kimeshindikana baada ya kupoteza 2-1 nyumbani, Stamford bridge.
Ilikuwa mechi nzuri ambayo PSG walianza mchezo taratibu kwa kuwa walikuwa na hazina ya ushindi wa 2-1 nyumbani, hivyo walipiga pasi fupi fupi na kumiliki eneo la katikati wakati Chelsea walijaribu kushambulia kwa kasi kwa staili ya mashambulizi ya kushtukiza. Lakini mechi ilikuwa ngumu zaidi baada ya kutanguliwa kufungwa goli na beki Rabiot kisha baadae kusawazisha kupitia Diego Costa.
Kipindi cha pili Zatlan Ibrahimovic alikata kabisa matumaini ya Chelsea baada ya kufunga goli la ushindi dakika ya 69.
Kuna kitu kimoja ambacho nilikiona kwenye mchezo huu, kitu ambacho kinaweza kuwa gharimu PSG kwenye hatua zinazofuata ambazo ngumu zaidi ya hii. Sote tuliona nafasi alizotengeneza Diego Costa mfano lile goli lake la kwanza pamoja na ile nafasi aliyokosa mapema kipindi cha kwanza
David Luiz aliacha nafasi kwa Diego Costa, akapigwa chenga kisha Costa kupiga shuti ambalo liliondolewa na mlinda mlango wa PSG. Baadae tena Thiago Silva aligeuzwa na Costa kwa staili ile ile akapiga shuti ambalo liliipa Chelsea goli la kusawazisha.
Uwezo wa Costa dhidi ya mabeki wa PSG ndiyo kitu ambacho kinanipa wasi wasi kuhusu nafasi yao kwenye hatua zinazofuata. Beki ya PSG inaacha mianya ambayo inatumiwa na timu pinzani kupata mabao. PSG kwenye hatua hii wameruhusu goli nyumbani pia wamefungwa tena ugenini.
Sio kama sikubali uwezo wa Costa jana, lakini naona udhaifu wa beki ya PSG kuacha mianya kwenye eneo la ulinzi kumechangia Costa kunga’ra. Wanacheza vizuri sana eneo la mbele na katikati mwa uwanja lakini bado matatizo kwenye ulinzi yatakuwa tatizo pindi wakikutana na washambuliaji hatari aina ya Lionel Messi, Lewandowski na Cristiano Ronaldo.
Kwa ufupi kocha Laurent Blanc anatakiwa kurekebisha makosa ya safu yake ya ulinzi kuepuka madhara ya baadaye kwenye michuano hii ikiwa anataka kuapata mafanikio.
Diego Costa alifanya vizuri kwenye mchezo wa jana, aliigeuza beki ya PSG takribani mara mbili na zote ilikuwa hatari kwa PSG. Lakini timu yake imeishia kutolewa kitu ambacho ni afadhali kwa mabingwa watetezi wa Ufaransa, madhara ya ubora wake tayari yameisha. Lakini udhaifu huu wa kina Thiago Silva na David Luiz bado ni tatizo kuelekea robo fainali.
Tags
MICHEZO KITAIFA