Nianze na nukuu hizi mbili kuntu za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere- Mwenyezi Mungu amrehemu.
“Democracy is not a bottle of Coca-Cola which you can import. Democracy should develop according to that particular country”.June 1991 in Rio De Janeiro, Brazil
"Demokrasia
sio chupa ya Coca-Cola ambayo unaweza kuagiza. Demokrasia lazima ikue na
kuendelezwa kulingana na nchi husika". Juni 1991 Rio De Janeiro, Brazil
(Tafsiri ni yangu)
“No nation
has the right to make decisions for another nation; no people for
another people”. From ‘A Peaceful New Year’ speech, Tanzania, January
1968
"Hakuna
Taifa lina haki ya kufanya maamuzi juu ya Taifa lingine; wala watu juu
ya watu wengine ". Hotuba ya Amani ya Mwaka Mpya, Tanzania, Januari 1968
(Tafsiri ni yangu)
Hili la
Marekani na uamuzi wa MCC ni jambo la mpito na haliwezi kuua mahusiano
yetu na Marekani. Tanzania na Marekani zinashirikiana kwa mambo mengi na
MCC ni sehemu tu tena ni eneo jipya la ushirikiano.
Uamuzi huu ni
jaribio kwa uhuru wa Taifa letu. Hakuna namna nyingine ila kushinda hili
kama tulivyoshinda mengine huko nyuma. Kwa wale ambao wameuona umri
watakumbuka namna tulivunja uhusiano na Ujerumani Magharibi 1964 pale
walipotaka kuwa na kauli hasi dhidi ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar.
Tulivunja
uhusiano na Ujerumani Magharibi baada ya kutaka kuingilia Uhuru wa
Mataifa Mawili huru yaliyoamua kuungana na kuunda Nchi Mpya ambayo leo
tunajivunia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1965 Tulivunja
uhusiano na Uingereza kufuatia na kitendo cha wazungu wachache
kujitangazia Uhuru (Unilateral Declaration of Independence) kule
Rhodesia na uingereza kukaa kimya na kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Tulivunja
Uhusiano na Uingereza kuieleza Dunia kwamba Uhuru wa nchi za Afrika ni
kipaumbele muhimu kwa Tanzania. Jambo tunalopaswa kufahamu ni kuwa MCC 2
toka mwanzo imekuwa ni mtihani dhidi ya uhuru wetu.
Napenda
ieleweke kwamba kipindi hiki kilichotokea sio kuvunjika kwa uhusiano
wetu na Marekani bali taasisi ya MCC ndio imesitisha msaada wao kwetu,
lakini mahusiano yetu na marekani bado yako pale pale, na si Marekani au
Tanzania inayoweza kuugharimu uhusiano wetu.
MCC 1 ilikuwa
ni chambo cha kutuvuta na tulipewa bila masharti tena hela nyingi dola
milioni 698 na ni fedha tulizopewa moja kwa moja na kupewa uhuru wa
kuamua tuzitumieje.
Tanzania
ilitakiwa kuainisha maeneo kisha wao wanatoa hela. Ndio maana miradi
kama ile barabara ambazo hazikuwa zikipata ufadhili kwa kuwa
hazikuonekana ni za kiuchumi na miradi ya maji ya Morogoro na kwingineko
iliingizwa humu na kupata ufadhili.
MCC 2 sio hivyo. Kwenye MCC 2 walengwa wakubwa ni sekta binafsi ya Marekani, hapa kuna mtego hapa, hapa ni biashara hapa.
Mchakato wa MCC
2 ulipoanzishwa, wafanyabiashara kwa kushirikiana na Maseneta
wakaanzisha hoja kuwa kwanini Marekani inatoa fedha kwa ufadhili katika
nchi ambazo China ndio wenye kufaidika na fedha hizo?
Wakaleta hoja
ya kuwa Serikali ya Marekani ifanye jitihada ya kuweka fedha kwa
kusaidia Sekta Binafsi ya Marekani kupenya Afrika.
Ukaitishwa
mkutano wa US-Africa Summit na agenda kubwa ikawa Power Africa. Katika
Power Africa, Marekani ikalichagua eneo la Nishati (si uzalishaji
viwanda) kwa kutambua kuwa ndio eneo pekee wanaloweza kushindana na
wachina.
Wakasema
wataelekeza fedha huko kuisaidia Afrika kutatua tatizo la nishati ambalo
ndio pembejeo ya viwanda. Wakaweka sharti kuwa fedha hizo na miradi
hiyo itatekelezwa na Sekta Binafsi ya Marekani.
Ndio sababu
wengi wenu mtakumbuka hata Rais Obama alitangazia dhamira ile pale
Ubungo kwenye Mitambo ya Symbion Power na sio kwamba alipenda kwenda
kutembea Ubungo.
Kuanzia hapo
kumekuwepo na shinikizo kubwa sana na masharti magumu na yenye
kuhamahama (shifting goal post) kutaka kuibaka sekta ya nishati nchini
ikiwemo mageuzi ya TANESCO.
Zikaainishwa
hatua kadhaa,ambazo utekelezaji wake baadhi ni kisheria na kisera na
hivyo haziwezi kwenda kwa deadline walizotaka.
Kila bodi
ikikutana wanaibua hiki na kile lakini wakisema hela watatoa. Hela hizi
zikawa zimeshikiliwa kama chambo ukisogelea zinasogea, ni sawa na ule
mchoro wa Mpanda Punde aliyeshika fimbo yenye majani na akiielekeza
mbele ya punda, kwamba punda ataendelea kuyafuata majani akidhani
atayafikia kumbe ndio anaupiga mwendo.
Hatimaye
wakasema wanasubiri uchaguzi mkuu jambo ambalo halihusiani na madai ya
mwanzoni. Baada ya uchaguzi wakaibuka na suala la Zanzibar.
Hivyo, uamuzi
wao wa leo ni uamuzi uliotarajiwa. Pia ni uamuzi wenye madhara kwa sekta
binafsi ya Marekani pia ambayo ndio ilikuwa itekeleze miradi hiyo.
Kama Taifa ni
muhimu kulinda utu na uhuru wetu. Ndio msingi wa sera yetu ya nje toka
mwanzo na hata sasa. Tumetofautiana na Marekani katika hili tutapatana
katika mengine. Ndio uhai wa maisha ya diplomasia.
Wao nao wanayo
hadhira ya wapiga kura wao wanayojaribu kuituliza huko nchini kwao kwa
uamuzi huu. Tunapaswa kuheshimu uamuzi wao kama ambavyo wanapaswa
kuuheshimu wetu.
Hatimaye baadae
tutapatana. Marekani inaihitaji Tanzania zaidi na Tanzania inaihitaji
Marekani. Marekani inahitaji MCC 2 zaidi hali kadhalika Tanzania
inahitaji MCC 2.
Mahusiano ya Tanzania na Marekani hayakuanza na hayataisha na MCC. MCC imeyakuta na itayaacha.
Kama marudio ya
uchaguzi wa Zanzibar ndio kigezo, basi Marekani isingekuwa inatoa zaidi
ya Dola Bilioni 3 kila mwaka kwa Egypt iliyo chini ya utawala wa
kijeshi kwa sababu ya kuununua ugomvi wa Egypt na Israel na isingetoa
kiasi cha dola bilioni 6 kwa Israel kila mwaka kwa yale wanayoyafanya
dhidi ya Wapalestina.
Huu ni wakati
ambao Taifa linawaita Wazalendo wake. Wazalendo wasimame na kusema 'Nchi
yangu KWANZA, iwe Sahihi au Imekosea" na Makuwadi watashangilia na
kusema "si mnaona sasa kiko wapi?".
Huu ni wakati
wa kujifunga mikanda na kulinda heshima yetu kama Taifa letu. Tuna
vyanzo vya mapato vingi sana ambavyo hatujaanza kukusanya mapato, tuwe
wabunifu na tusibweteke na kutegemea mapato yataongezeka maradufu kwa
vyanzo vile vile.
Niseme kwa
uchache, sababu walizotoa MCC, na ieleweke aliyetoa tamko ni MCC, heri
lingetoka tamko hili Wizara ya Mambo ya Nje au Ikulu ya Marekani, moja
ni Zanzibar na pili ni Sheria ya Makosa ya Mitandao (Cyber crimes Act).
Sasa hebu tujadili kidogo, hivi kule Zanzibar tulitaka kitokee nini pale ambapo wanasiasa walikuwa hawataki kujadiliana?
Tume ile ile ya
Uchaguzi ambayo bado ilikuwa na uhalali wa kikatiba na kisheria
kuuitisha, kuufuta na kuuitisha tena uchaguzi ikachukua nafasi yake.
Wanasiasa wasio
makini wakaishia kuhamishia malumbano mitandaoni badala ya kuitafuta
suluhu ya kisiasa na pale siasa iliposhindikana basi wangeitafuta suluhu
katika mahakama za Zanzibar.
Mezani
wakashindwa, mahakamani hawakwenda. Tume ikachukua uongozi, uchaguzi
ukaitishwa Wananchi wakapiga kura na sasa huko Zanzibar kuna serikali na
baraza la wawakilishi.
Hata mimi
sifurahii sana njia waliyoichukua Zanzibar lakini ilibidi siasa za
madaraka zisite ili tuanze kufanya siasa za maendeleo. Je wamarekani
walitaka muujiza gani utokee huko.?
Kuhusu Sheria
ya Mitandao, hata mimi siipendi, si twende mahakamani, bunge litaanza
vikao muda si mrefu je wabunge si wapeleke hoja ya kuifanyia marekebisho
sheria hii.
Sasa Marekani (MCC) inapoweka shinikizo kwa suala la Sheria ambayo ni jambo la ndani na linaloweza kujadilika, sijaelewa.
Mbona sie
hatujapiga kelele Yule jamaa yao Trump alipotutusi waafrika na kusema
sisi stahili yetu ni kuwekwa tena chini ya ukoloni (hapa nimechomekea
tu).
INDHARI
Ni aibu kwa
viongozi wa kisiasa kufurahia jambo hili, ni ishara ya ukuwadi wa
kisiasa na ambao uko tayari kukumbatia mahusiano yanayotweza Uhuru wetu.
It is now high time kufanya siasa safi za maendeleo (politics of
development) na sio kujikita katika katika siasa za madaraka (Politics
of Power).
*************
Imeandikwa na: Humphrey Polepole.
Mwandishi, Ndg.
Humphrey Polepole amenufaika na uelewa wa watu wenye uzoefu wa
mahusiano ya Tanzania na nchi za Nje. Aidha, ni mnufaikaji (alumni) wa
programu ya uongozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Tags
UCHAMBUZI
