Mahmoud Ahmad Monduli
Monduli, Baraza la Madiwani wa
Halmashauri ya Monduli mkoa wa Arusha, limetangaza kujiondoa kutengeneza
magari yake,wakala wa serikali wa ufundi na umeme(TEMESA), kutokana na
gharama kubwa ya vipuri tofauti na bei halali za soko.
Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya ya Monduli, Isack Joseph alitoa maamuzi hayo, baada ya kupokea
taarifa ya matengenezo hafifu na malipo makubwa ya magari ambayo
ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,
Ephraem Ole Nguyaine.Joseph
alisema haiwezekani TEMESA wawauzie kioo(wind Screen) cha gari kwa sh
900,000 wakati kioo hicho kinauzwa sh. 300,000 na pia wamefanya
matengenezo kwa ya magari kwa sh 2 milioni hadi milioni 3 wakati
matengenezo hayo gharama yake ni kati ya 600,000 na Sh1 milioni.
“huu ni mfano hai na gharama hizi, zimetumika katika gari STK 2223 na tuna risiti zote jambo ambalo tunaamini ni wizi”alisema.
Mwenyekiti huyo, alisema wao
waliamini TEMESA kwa kuwa ni taasisi ya serikali ingefanyakazi nzuri
lakini wao sasa ndio wamekuwa tatizo na kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu.
Awali Mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Ole Nguyaine alisema tayari ameandika barua ya malalamiko hayo
kwenda kwa katibu Tawala mkoa wa Arusha na TEMESA makao makuu,
kulalamikia malipo ya matengenezo hafifu.
Katika barua hiyo, pia
halmashauri hiyo, imelalamikia tatizo la kuchelewa kutengenezwa magari
kutokana na kutaka kuliwa kabla hali ya kuwa mfumo wa malipo ya
halmashauri kwa sasa haiwezekani.
“pia TESEMA wanakataa kujaza fomu
za TIMS pamoja na matengenezo kufanyika kwao, hali ya kuwa halmashauri
zinatakiwa kufuata utaratibu wa TIMS kwenye matengenezo ya
magari”alisema
Kutokana na mapungufu hayo,
baraza hilo limeagiza halmashauri kutafuta utaratibu mwingine wa
kutengeneza magari ambao unapunguza matumizi ya fedha za umma yasiyo ya
lazima ili fedha hizo zifanye kazi ya maendeleo.
Hata hivyo, hakuna afisa wa
TEMESA mkoa wa Arusha ambaye alikuwa tayari kuzungumzia malalamiko hayo,
kwa maelezo kuwa barua za malalamiko zipo ngazi za juu.
Tags
HABARI KITAIFA