BANDA MEDIA BLOG

SI TU KUONGOZA LIGI, YANGA SC WANAONGOZA PIA KATIKA HILI, SPORTS IKIWA TAABAN

Kikosi cha Yanga kilichoanza dhidi ya Azam FC
Kikosi cha Yanga kilichoanza dhidi ya Azam FC
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam
Yanga SC inaongoza msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara (kabla ya mechi ya Simba v Ndanda, leo Alhamis) lakini mabingwa hao watetezi si tu wamekusanya alama nyingi zaidi (pointi 50) baada ya kucheza mechi 21 bali wanashikilia pia chati ya ufungaji na sifa ya timu yenye beki ngumu zaidi hadi sasa.
Yanga wamefanikiwa kufunga jumla ya magoli 51, na kuruhusu nyavu zao mara 11 tu. Mshambulizi wa timu hiyo Amis Tambwe tayari amefunga magoli 17, na kwa karibu anafuatiwa Hamis Kizza wa Simba SC aliyekwishafunga magoli 16.

Simba inafuatia kwa ufungaji, katika michezo 21 wamefunga jumla ya magoli 37 (magoli 14 pungufu ya Yanga.) ‘Wekundu wa Msimbazi’ wameruhusu magoli 13 sawa na timu za Azam FC na Mtibwa Sugar FC. JKT Ruvu ya Pwani ambayo iliwachapa 2-0 Toto African siku ya jana Jumatano ndiyo timu iliyofungwa magoli mengi zaidi katika VPL hadi sasa.
Kikosi hicho cha mkufunzi Abdallah ‘King’ Kibadeni kipo katika nafasi ya 12 kimeruhusu jumla ya magoli 35 katika michezo 22. Majimaji FC iliyo nafasi ya 11 inafuatia kwa karibu ikiwa imeruhusu magoli 32.
African Sports ya Tanga yenyewe ndiyo timu iliyofunga magoli machache zaidi hadi sasa. Katika michezo 22 timu hiyo imefanikiwa kufunga jumla ya magoli 7. Majimaji pia ni dhaifu katika ufungaji kwani imefunga magoli 12 tu katika michezo yake 22.
Magoli 13 ya mshambulizi wa Yanga, Donald Ngoma yanalingana na yale yote yaliyofungwa na timu ya Kagera Sugar. Kikosi cha Richard Adolf kilifanikiwa kufunga goli lake la 13 jana Jumatano katika sare ya kufungana 1-1 na Tanzania Prisons katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Stand United, Ndanda SC, Toto Africans zimefunga magoli 19 kwa kila timu. Mtibwa imefunga magoli 24 katika michezo 20 waliyokwisha cheza, JKT Ruvu licha ya kuwa timu iliyoruhusu magoli mengi zaidi hadi sasa, lakini katika ufungaji wapo nafasi ya 5 wakiwa wamefunga jumla ya magoli 22.
Prisons imefungana na Mwadui FC kwani timu zote mbili zimefunga magoli 21 wakati timu za Ndanda na Stand zimefungana zikiwa zimefunga magoli 19 kila timu.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG