Na Fatma Salum (MAELEZO)
Wanawake nchini wamehimizwa
kushiriki kwenye michezo mbalimbali kuanzia ngazi ya vijiji hadi taifa
ili kuboresha afya zao na kujiongezea kipato.
Hayo yamesemwa na Waziri Ofisi
ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Kazi Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama
leo jijini Dar es Salaam wakati akihutubia kwenye Tamasha la Michezo kwa
wanawake lililoandaliwa na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuelekea
kilele cha Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 kila mwaka.
Akihutubia kwa niaba ya Makamu
wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Jenista ameeleza kuwa Serikali
ina mipango thabiti ya kuboresha sekta ya michezo hivyo ni wakati
muafaka kwa wanawake wa rika zote kushiriki kwenye michezo kwa manufaa
yao na taifa kwa ujumla.
“Wanawake tunaweza tusisubiri
kuwezeshwa tujitokeze kwenye michezo kuanzia kwenye maeneo tunayoishi
kwani itatusaidia kuimarisha afya zetu na kuepuka majanga ikiwemo UKIMWI
hasa kwa wasichana kwa kuwa wanaposhiriki kwenye michezo wanaepuka
kujihusisha na vitendo viovu kama ulevi na uasherati vinavyopelekea
maambukizi” alisema Mhe. Jenista.
Aidha Mhe. Jenista amelitaka
Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kuandaa program maalum za kuhamasisha
makundi mbalimbali kushiriki kwenye michezo hasa wanawake, watoto na
walemavu.
Pia Mhe. Jenista ametoa wito
kwa wadau wa michezo ikiwemo Mifuko ya Hifadhi za Jamii kushirikiana na
BMT kuandaa matamasha mengi ya michezo yatakayohusisha wanachama wa
mifuko hiyo ili kuimarisha afya zao na kuepuka maradhi kama Shinikizo la
Damu na Kisukari yanayosababisha mifuko hiyo kutumia gharama kubwa
kuwatibia kupitia fao la matibabu.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa BMT Mhe. Zainab Vullu (Mb) ameiomba Serikali kutatua
changamoto zinazoikabili sekta ya michezo ikiwemo kupunguza kodi kwa
vifaa vya michezo vinavyoingia nchini na kuboresha mitaala ya elimu ya
michezo mashuleni.
Tamasha hilo la michezo kwa
wanawake limefanyika katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam
likibeba kauli mbiu ya mwaka huu inayosema ” 50 kwa 50 ifikapo 2030,
Tuongeze Jitihada, Maendeleo ya Wanawake kupitia Michezo Inawezekana”.
Tags
HABARI KITAIFA