Na Baraka Mbolembole
LICHA ya kuwa nyuma kwa alama 8 dhidi ya vinara Simba SC katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara, mkufunzi mkuu wa Yanga SC, Hans Van der Pluijm amesema kikosi chake bado kina nafasi ya kufanya vizuri msimu huu.
Hans amesema hayo siku ya Jumatatu nilimpofanya naye mahojiano mafupi.
“Haifurahishi kwa kweli, wachezaji wetu wamechoka sana na inabidi tuwe makini kwa hili.” anasema kocha huyo mshindi wa mataji mawili ya VPL na moja la FA.
“Pointi tatu katika kila mchezo ndicho wanachohitaji wapenzi wa Yanga, na mimi nahitaji pia. Tulikuwa na uwezo wa kumaliza mechi ndani ya kipindi cha kwanza (akimaanisha game ya Azam FC 0-0 Yanga siku ya Jumapili iliyopita) kama tungetumia vizuri nafasi tulizozipata.”
“Kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri upande wetu, kipindi cha pili hakikuwa kizuri. Azam walitawala mpira muda mwingi.” anasema kocha huyo ambaye timu yake itakuwa ugenini kuwavaa Toto Africans ya Mwanza siku ya kesho Jumatano katika uwanja wa CCM Kirumba.
Baada ya kuangusha alama 9 katika game 8 za mwanzo msimu huu nilimuuliza Hans kama kikosi chake kinaweza kushinda ubingwa msimu huu.
“Ilishawahi kutokea kwa Manchester United, Manchester City na pia timu nyingine, bado kuna mechi nyingi za ligi. Mashabiki wanatakiwa wawe wavumilivu na waisapoti timu pia katika kipindi hiki kigumu. Hicho ndicho timu yetu inachostahili.”
Endelea kufuatilia website hii kwa maelezo zaidi kuhusu Hans na Yanga.
Tags
MICHEZO KITAIFA