Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa mamlaka ya maji Lindi Mhandisi Adam
Alexanda aliyeshikilia makabrasha kutokana na kushindwa kusimamimia
ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika manispaa ya Lindi pamoja na
matumizi mabaya ya ofisi, Waziri mkuu amemuelekeza Mkuu wa Kupambana na
rushwa TAKUKURU mkoani Lindi kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za
Mhandisi huyo.
Picha na Chris Mfinanga
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander akisikiliza maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
…………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA),
Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na
kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa
ya Lindi.
Waziri Mkuu amemkabidhi Mhandisi
huyo kwa Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Lindi, Bw. Stephen Chami na
kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Oktoba 19, 2016) wakati alipotembelea mradi wa maji wa
Ng’apa ambapo ameagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa
mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.
“Kamanda wa TAKUKURU fanya
mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa Wizarani, mimi
najua analipwa na LUWASA. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es
Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Mhandisi hiyo anakabiliwa na
tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na
kupokea mshahara bila la kulipa kodi ya mapato ya mshahara (PAYE),
kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu amesema Serikali
haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa
dhamana ya kuwatumikia hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi. “Huyu
nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam.”
Alipoulizwa sababu za kutokuwepo
ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar
es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatulia changamoto
mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.
“Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal
na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa
posho tu! Tena baada ya kulipwa sh.120,000 kwa siku wewe unajilipa
sh.150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” amesema.
Waziri Mkuu amemaliza ziara yake siku tatu mkoani Lindi na amerejea jijini Dar es Salaam.
Tags
HABARI KITAIFA