Kondakta wa daladala linalofanya safari zake kati ya Nguvumali hadi
Raskozone, Salim Kassim amefariki dunia baada ya kudaiwa kushambuliwa
ndani ya kambi ya jeshi jijini hapa.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba, kondakta huyo alikufa
wakati akipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo na chanzo cha kifo
bado kinachunguzwa.
Mwananchi ilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku, ambapo
mashuhuda walidai kuona kondakta huyo akichukuliwa na wanajeshi na
kuingizwa kambini na baadaye alitolewa akiwa hajitambui
Akizungumzia tukio hilo, Khalid Juma mkazi wa Nguvumali jijini hapa
alisema askari hao wamekuwa na desturi ya kuwapiga wananchi bila
kuchukuliwa hatua zozote za kisheria.
“Tumekuwa tukipata vipigo kila wakati, licha ya viongozi kupata taarifa
za matukio hayo wamekaa kimya na hili tukio ni la tatu kutokea hapa,”
alidai Khalid.
Diwani wa Kata ya Nguvumali ambaye pia ni Meya wa Jiji la Tanga, Alhaji
Mustapha Selebosi alisema sababu za kipigo hicho ni mwanafunzi wa shule
moja jijini Tanga ambaye ni mtoto wa ofisa wa JWTZ kuzozana na kondakta.
Tags
UKATILI
