Katibu wa waumini wanaomuunga mkono Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana
Tanzania, Dk Jacob Chimeledya, Thomas Gambo amesema kinachompa kiburi Dk
Valentino Mokiwa ni kuungwa mkono na baadhi ya mapadri, makasisi na
mashemasi ambao aliwawekea mikono akiwa askofu wa Dayosisi ya Dar es
Saalam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake jana, Gambo alisema Dk Chimeledya
atafanya ibada ambayo itahusisha kumsimika Naibu Askofu wa Dayosisi ya
Dar es Salaam, itakayoamua mustakabali wa mgogoro wa uongozi uliopo.
Ibada hiyo itafanyika Kanisa Kuu la Dar es Salaam. Hata hivyo,
hawakutaja siku bali alisema katika ibada hiyo, Askofu Chimeledya
atafanya mambo mbalimbali ikiwamo kutangaza kubadilisha uongozi wa
dayosisi na kuwapa upya viapo mashemasi na mapadri.
Dayosisi ya Dar es Salaam imekuwa katika mgogoro tangu Askofu
Chimeledya amtake kiongozi wake, Dk Mokiwa ajiuzulu kwa madai kuwa
anatumia madaraka yake vibaya na tuhuma za ubadhirifu.
Hata hivyo, Dk Mokiwa alikataa kujiuzulu, akisema mkuu wake alikiuka
taratibu ikiwamo kufanya uamuzi ambao uko chini ya mamlaka ya dayosisi
na kutopeleka uamuzi huo kwenye Nyumba ya Maaskofu kama taratibu
zinavyotaka.
Gambo alisema: “Siku hiyo tutawajua mashemasi na mapadri wanaomuunga mkono Askofu Chimeledya na Dk Mokiwa.”
Tags
HABARI ZA DINI