Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ametolea ufafanuzi kuhusu
hatua inayochukuliwa na vyombo vya dola dhidi ya watu wanaohusika na
vitendo vya unyanyasaji vikiwemo kupiga watu.
Naibu waziri huyo ametoa ufafanuzi huo Jumatano hii mjini Dodoma kwa
niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, wakati alipokuwa akijibu swali la
mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi.
Mbilinyi aliuliza, “Kumekuwa na tabia za watu kupiga watu wengine,
vipigo ambavyo vinafikia kiasi cha utesaji matukio kama yaliyotokea
Mbeya Day sekondari kwa mwalimu kumshambulia mwanafunzi lakini na lile
la mtu kumtoa macho mwingine tukio lililotokea kule Buguruni, Je,
Serikali inachukua hatua gani kwa watu wanaowapiga wenzao bila sababu?”
Mheshimiwa Masauni alijibu, “Ni kweli hivi karibuni kumekuwa na vitendo
vya kusikitisha katika nchi yetu na kwa jamii ambavyo ni kinyume na
sheria na havikubaliki. Aidha serikali haikubaliani na vitendo vya namna
hiyo vinavyofanywa na watu, mtu au kikundi kwani vitendo hivyo ni
kinyume na sheria na utaratibu mzima wa haki za binadamu. Serikali
kupitia jeshi la polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuzuia na
kulinda raia na mali zao, aidha serikali kupitia jeshi la polisi
tumepokea taarifa za matukio mbalimbali na kuyafanyia uchunguzi wa kina
yanapobainika upo ushahidi wa kutosha mtuhumiwa huchukuliwa hatua za
kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.”
Aliendelea, “Nichukue fursa hii kuwaasa wale wote wanaokiuka taratibu,
kanuni na sheria za nchi waache tabia hiyo mara moja wizara yangu
haitakuwa na suluhu kwa mtu yeyote atakayetenda uhalifu huo.”
Ameongeza “Kuhusiana na suala la walimu ambao wamewanyanyasa wanafunzi
kwenye shule ya Mbeya day, suala hili ni suala mtambuka kwahiyo ni hatua
mbalimbali zinachukuliwa na mamlaka husika kwa upande wa jeshi la
polisi kwa kushirikiana na mkurugenzi wa mashtaka ni kwamba kuna hatua
zinaendelea kuchukuliwa na pale ambapo uchunguzi utakamilika
watafikishwa katika vyombo vya sheria.”
Tags
ELIMU
