Mmoja wa wachimbaji waliokolewa
katika ajali ya kifusi akimweleza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (kulia) jinsi ajali hiyo ya kufikiwa na kifusi
wachimbaji 18 ilivyotokea. Katikakti anayesikiliza ni Kaimu Kamishna wa
Madini Mhandisi Ally Samaje.
Mmoja wa wachimbaji wadogo
akishuka chini ya shimo la kuingilia katika mgodi kwa ajili ya kusaidia
shughuli za uokoaji kufuatia ajali ya kufukiwa na kifusi wachimbaji 18
katika eneo la Buhemba mkoani Mara.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Mgodi wa
North Mara (ACACIA) ambao walishiriki katika zoezi la uokoaji wa
wachimbaji wadogo kwa kutoa msaada wa mashine ya kuvuta maji na tope
ili kuwezesha zoezi la ufukuaji kuendelea
Sehemu ya Wachimbaji wakifuatilia
mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati
wa ziara yake katika mgodi wa Buhemba unaomilikiwa na STAMICO.
Mmoja wa wachimbaji wadogo
anayeshiriki zoezi la uokoaji katika eneo la Buhemba akimweleza Waziri
wa Nishati na Madini , Profesa Sospeter Muhongo na wananchi waliokuwa
eneo hilo kuhusu hali ilivyo ndani ya mgodi huo.
Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo akiongea na wachimbaji wadogo katika eneo la
Buhemba ambapo ajali ya wachimbaji wadogo walifukiwa na kifusi tarehe 13
Februari,2017.
Serikali imesema itatoa eneo
linalomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Buhemba, Mkoani
Mara kwa wachimbaji Wadogo wa Madini baada ya kufanyika kwa tathmini na
taratibu za kumilikishwa eneo ili wachimbaji hao wafanye shughuli hizo
kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu ikiwemo kulipa kodi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo leo tarehe 18 Februari,2017,
wakati wa ziara yake katika mgodi huo ili kuangalia shughuli za uokoaji
zinazoendelea katika mgodi huo, kufuatia ajali ya kufukiwa na kifusi
kwa Wachimbaji 18 iliyotokea tarehe 13 Februari,2017, ambapo wachimbaji
13 waliokolewa siku hiyo hiyo
Prof. Muhongo amesema kuwa,
wachimbaji hao hawakuwa na leseni wala vibali halali vilivyotolewa kwao
kufanya shughuli za utafutaji dhahabu na kwamba eneo hilo linamilikiwa
kisheria na STAMICO kwa leseni PL N0. 7132/2011, na kuongeza kuwa,
wachimbaji hao walivamia eneo hilo ambapo ni kosa kisheria na
wanatambulika kama wavamizi.
Ameongeza kuwa, shughuli za
uchimbaji katika eneo hilo zilifungwa tangu mwaka 1971 ambapo awali eneo
hilo lilikuwa chini ya wakoloni kabla ya kuwa chini ya uangalizi wa
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kampuni ya Meremeta na baadaye kuwa chini
ya umiliki wa STAMICO.
Aidha, amezuia shughuli zote za
uchimbaji kufanyika katika eneo hilo na kusema kinachofanyika sasa ni
kuutafuta mwili wa mchimbaji mmoja ambaye bado haujatolewa. ”Hadi sasa
wachimbaji 15 wamekwisha okolewa, bahati mbaya wawili walitolewa
wamefariki na sasa tuendelee na zoezi la kutafuta mwili
uliobaki,”ameongeza Prof. Muhongo.
Pia Prof Muhongo amewshauri
wachimbaji hao kujiunga katika vikundi na kusajili vikundi hivyo ili
kuwezesha shughuli zao kufanyika kwa kuzingatia taratibu za uchimbaji.
“Jiungeni katika vikundi , lakini ni marufuku kwa familia moja kuwa na
kikundi,”amesisitiza Prof. Muhongo
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi
wa Madini Kanda ya Viktori Mashariki Mhandisi Juma Sementa amesema kuwa,
tayari Kanda hiyo imeshatoa maeneo yapatayo 35 kwa wachimbaji wadogo
katika eneo la Lwabasi, mkoani humo na kueleza kuwa, leseni zote katika
eneo hilo zinamilikiwa na wachimbaji wadogo na hivyo kuwataka kufanya
shughuli za uchimbaji kwa kuzingatia usalama na ikiwemo kulipa kodi.
Tags
HABARI KITAIFA