Bila shaka kila mmoja wetu anakumbuka ahadi ya RC Makonda aliyoitoa
mwaka jana ya kujenga viwanja vitatu (3) vya mpira kwa ajili ya
maendeleo ya mashindano mbalimbali ya michezo ikiwemo Ndondo Cup kwani
mashindano haya kwa ujumla wake yanalenga kuboresha mazingira ya michezo
na kuzalisha vipaji vingi zaidi ambavyo vinabeba ajira nyingi za vijana
ndani yake.
Kimsingi RC Makonda hakuishia tu kuahidi bali alikwenda mbali zaidi na
kumualika Balozi wa China nchini Tanzania, Dr. Lu Youqing kushuhudia
hali halisi ya viwanja vinavyotumika kwa sasa kama sehemu ushahidi wa
kile alichokuwa amemueleza wakati akimshawishi.
Ikiwa imepita miezi kadhaa tangu Balozi kukubaliana na ombi la Mkuu wa
Mkoa, jana Machi 3, 2017 Balozi huyo wa China akiwa na RC Makonda
wameweka historia mpya baada ya kuweka jiwe la msingi la kuanza ujenzi
wa viwanja hivyo, huku wakianza na kiwanja cha Bandari ambacho
kitagharimu Dola za Kimarekani 450,000, huku kikijengwa kwa viwango vya
kimataifa na kampuni iliyojenga uwanja wetu wa taifa.
Kuonyesha kutambua utendaji na msukumo mkubwa wa RC Makonda katika
kutimiza azma ya Rais John Pombe Magufuli ya kutatua changamoto za
wanyonge, Balozi pia amemuahidi Mkuu wa Mkoa kufanya yafuatayo:
1. Kuwapatia kipaumbele cha ajira vijana wote watakaoshiriki mashindano
ya Ndondo Cup kwenye kampuni mbili za nchi hiyo ambazo zinatarajia
kuanza shughuli zake hivi karibuni huku wakitarajia kuajiri zaidi ya
vijana 24,000
2. Kuipeleka nchini China timu itakayoshinda michuano hiyo ili ikacheze
mechi za kirafiki kama sehemu ya kuwaongezea ujuzi wa soka.
3. Kama haitoshi, timu ya pili na ya tatu kwenye mashindano zitapewa mualiko rasmi kwenye ubalozi wa nchi hiyo.
Kwa namna ya kipekee RC Makonda amemshukuru Balozi huyo kwa kuwa sehemu
ya watu ambao wamechangia maendeleo ya jiji la Dar es Salaam na hivyo
shughuli za maendeleo ambazo hazikuwepo kwenye bajeti ya serikali kuweza
kufanyika pia.
Tags
MIUNDOMBINU
