Rais John Magufuli amemuagiza DC Bagamoyo kuwasaka, kuwakamata na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria wafugaji wote wanaodaiwa kuhusika
katika matukio ya kuwashambulia kwa viboko wananchi wa Kijiji cha
Fukayosi kilichopo Wilayani humo.
Mhe. Dkt. Magufuli aliyekuwa akisafiri kwa gari kutoka Dodoma kwenda
Jijini Dar es Salaam ametoa agizo hilo leo tarehe 17 Machi, 2017
aliposimama katika kijiji hicho baada ya kuona wananchi wengi wakiwa
wamekusanyika kando ya Ofisi ya Kata.
Baada ya kusimamisha msafara wake, Mhe. Rais Magufuli aliwaita wananchi
waliokuwa wamekusanyika huku wakiwa wameshika mabango yaliyoandikwa
ujumbe wa kutaka wafugaji wa jamii ya Wamang’ati waondolewe na kisha
akatoa nafasi kwa baadhi yao kueleza dukuduku lao.
Wananchi hao ambao ni wakulima na mfugaji mmoja aliyejitokeza wakaeleza
kuwa Wamang’ati wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuingiza mifugo katika
mashamba yao ya mazao na wakithubutu kuwakataza wamekuwa wakichapwa
viboko na baadhi kuuawa.
Katika majibu yake, pamoja na kutaka wote wanaodaiwa kuwashambulia
wananchi kwa viboko wakamatwe Mhe. Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Wilaya
ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga kukomesha mara moja vitendo vya
wafugaji kuwapiga wakulima na wakulima kuwapiga wafugaji, na pia
kukomesha vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya
wakulima.
“Kuanzia leo isitokee mfugaji kumpiga mkulima, mkulima kumpiga mfugaji
wala mfugaji kulisha mifugo yake kwenye mashamba ya wakulima, na suala
hili nitalifuatilia mimi mwenyewe.
“Kwa hiyo Mkuu wa Wilaya na Viongozi mlishughulikie hili kabla mimi
sijawashughulikia nyinyi, wale waliopiga watu, nataka wote wakamatwe na
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Tags
RAIS MAGUFULI