WAKATI Simba ikiwa imesaliwa na mechi sita kabla ya kumaliza msimu wa
Ligi Kuu Bara, klabu hiyo imeanza kuumiza vichwa kufuatia majembe yake
matatu kugoma kusaini mkataba mpya. Majembe hayo ambayo yanategemewa
katika kikosi cha kwanza, mikataba yao inafikia tamati mwishoni mwa
msimu huu
ambapo kwa sasa viongozi wanahaha kuhakikisha wanawabakisha kikosini
hapo kwa misimu mingine ijayo. Wachezaji hao ni Ibrahim Ajibu, Jonas
Mkude na Abdi Banda ambapo imeelezwa kuwa viongozi wamepata ahueni
kidogo kwa Banda ambaye kwa sasa ndiye wapo naye kwenye mazungumzo ya
kumpa mkataba.
Akizungumza Ijumaa, bosi mmoja kutoka ndani ya Simba ambaye hakutaka
kuweka wazi jina lake, alisema wachezaji hao pekee ndiyo mikataba yao
inafikia tamati mwishoni mwa msimu huu lakini bado hawajaonyesha dalili
za kuongeza. “Hadi sasa wachezaji ambao wanatarajia kumaliza mikataba
yao hapa Simba ni watatu tu ambao ni Banda, Mkude na Ajibu, lakini wote
waliobakia wapo vizuri kwa kuwa mikataba yao ni ya muda mrefu.
“Kwa upande wa Mkude na Ajibu wenyewe tayari walishagoma kuongeza
mkataba kuendelea kubaki Simba licha ya uongozi kuwafuatilia, hivyo
tumeamua kuwaacha hadi hapo mikataba yao itakapoisha na kujua nini cha
kufanya, lakini Banda mazungumzo yanaendelea na huenda akaongeza mkataba
mwingine,” alisema bosi huyo.
Tags
SIMBA SC
