Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, ametoa wito wa kupunguzwa kwa mishahara ya
wabunge na maafisa wakuu akisema viwango vya juu vya mishahara
vimesababisha migomo ya wafanyakazi wa sekta nyingine kutaka nyongeza za
mishahara.
Rais Kenyatta ameyasema hayo alipohutubia kwenye kikao cha pamoja cha
Bunge la Taifa na Baraza la Senate katika hotuba yake ya mwisho ya
kipindi chake cha kwanza uongozini.
Hotuba ya Rais huyo imesheheni majibu ya maswali yanayoulizwa na
upinzani kila siku kuanzia ufisadi, ufujaji wa fedha za umma, kuzorota
kwa huduma za afya, elimu na usalama.
Rais Uhuru amejivunia kupungua kwa visa vya mashambulizi ya kigaidi
nchini, kuongezwa kwa idadi ya maafisa wa usalama na ukuaji wa uchumi
ambao amesema umekuwa juu ya kiwango cha makadirio ya taasisi za
kimataifa cha 3% kwa Mwaka.
Huku zikiwa zimesalia siku 145 kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika Rais
Kenyatta ametumia fursa ya hotuba hiyo kujipigia upatu ili aweze
kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili.
Rais Kenyatta amesema kwamba serikali yake imejitolea kuhakikisha
uchaguzi huru na haki na kuiomba Idara ya Mahakama kutotatiza
matayarisho ya uchaguzi ujao.
Tags
SIASA ZA NJE
