
Diwani wa CHADEMA Kata ya Kitwiru katika Manispaa ya Iringa Ndugu.
Baraka Kimata, alishikiliwa kwa muda na Jeshi la Polisi baada ya kutoa
maneno yaliyotafsiriwa kwamba ni kashifa kwa mbio za Mwenge. Kimata
ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa CHADEMA Iringa Manispaa aliitwa Jukwaani
kuongea kwa niaba ya chama chake baada ya Katibu wa CCM wilaya kuongea.
Kimata pamoja na mambo mengine aliyoongea, alimalizia hotuba yake kwa
kusema kwamba kama CHADEMA ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi basi
wataupumzisha Mwenge wa Taifa. Baada ya hapo wasemaji wote waliofuatia
akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Iringa na Mkimbiza Mwenge Kitaifa
walimshambulia Kimata na chama chake kwa msimamo huo wa kupinga Mbio za
Mwenge.
Baadaye Kimata alikamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kuhojiwa
na kuachiwa. Habari toka kwa watu walio karibu naye wanadai kwamba
Kimata ametakiwa kuandika barua ya kuomba radhi kabla ya kesho saa kumi
jioni.