Tanzania na Uganda zimefungua sura
mpya ya ushirikiano baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo
kusaini nyaraka inayoainisha maeneo mbalimbali ambayo nchi hizo
zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua uchumi wa mataifa yao.
Nyaraka hiyo iliyosainiwa leo
jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume ya Kudumu ya Pamoja ya
Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na Uganda kilichofanyika kwa siku
tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017.
“Makubaliano haya yataongeza
chachu ya uhusiano na ushirikiano wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa
kufanya kikao cha JPC tokea mkataba uliposainiwa mwaka 2007 nchini
Uganda”. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga.
Kikao cha JPC kilifanyika kwa
kuzingatia makundi ya kisekta ambapo katika kila kundi, wajumbe
waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote ambayo yanajumuisha
pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu; kilimo; viwanda;
biashara; uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira; uvuvi;
ufugaji; afya; elimu; utangazaji; madini na masuala ya kijamii.
Kikao hicho kilitarajiwa
kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita lakini kutokana na mashauriano
ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika, mikataba miwili ndio
iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika kuendeleza mradi
wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo na
huduma za usafiri wa anga.
Mikataba minne iliyosalia ambayo
inahusu ushirikiano katika usafiri wa reli, usafiri wa majini;
utangazaji na ulinzi wa raia itasainiwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa
Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) utakaofanyika hivi karibuni
hapa nchini.
Waziri Mahiga alieleza kuwa
kusainiwa kwa mikataba hiyo ni muhimu kwa kuwa itaimarisha zaidi
misingi ya mahusiano yetu, hivyo alizihimiza pande zote kukamilisha
mashauriano hayo ili mikataba hiyo iweze kusainiwa katika muda
uliopangwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo
ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa alisisitiza umuhimu wa Tanzania na
Uganda kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua uchumi kwa madhumuni ya
kuwaondolea umasikini wananchi.
Alisema mradi wa ujenzi wa bomba
la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ni moja ya
miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, hivyo alisisitiza
umuhimu wa kukamilisha taratibu zote zilizosalia ili ujenzi huo uweze
kuanza.
Alihitimisha hotuba yake kwa
kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa kufanikisha uwekaji saini wa mikataba
miwili ukiwemo wa kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14
katika eneo la Kikagati/Murongo ambao ulikuwa katika majadiliano kwa
zaidi ya miaka minane.
Kikao hicho cha JPC kimefanyika
kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa wakati wa ziara ya
Rais wa Uganda nchini mwezi Februari 2017. Viongozi hao waliagiza kikao
cha JPC kifanyike kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambao ulipangwa kufanyika jijini Dar Es Salaam
tarehe 06 Aprili 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 05 Aprili, 2017
Tags
BARA ZNZ