
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea kuwabana wala rushwa na
wanaoghushi risiti za ukusanyaji maduhuli kwa kuboresha mfumo wa
kieletroniki wa utumiaji wa mashine za (EFD) utakaowezesha miamala na
risiti kuwa na saini za kieletroniki.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Neema Mrema, aliyasema hayo jana jijini Dar
es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa ajili ya taasisi na mashirika ya
umma.
Mrema alisema hivi karibuni mawakala wa mashine za kieletroniki za
kutumia risiti watawafungia mfumo huo taasisi na mashirika hayo ili
wakusanye maduhuli kupitia mashine hizo.
Aidha, alisema TRA imefanya mabadiliko katika mfumo wa usimamizi wa
matumizi ya mashine za kieletroniki za utoaji risiti (EFDMS) pamoja na
mashine za EFD ili kupunguza gharama kwa serikali.
Alisema mfumo huo wa kielektroniki utaipunguzia serikali gharama za
kununua mashine halisi kwa kuwa umeunganishwa na mfumo wa kuhifadhi
taarifa wa TRA.
“Una usalama wa hali ya juu kwani miamala na risiti zote itakuwa na
saini ya kieletroniki … hivyo kunapunguza uwezekano wa kughushi risiti
kutoka kwenye mashine ambazo hazijasajiliwa na mfumo wa TRA,” alisema.
Pia alisema mfumo huo ni wa kiintelejensia kutokana na kuwa na uwezo wa
kutambua hati ya mauzo kwa mkopo, marejesho ya mauzo, risiti halali na
za kudurufu.
Kadhalika, alisema mfumo huo ni rafiki na unaweza kuunganishwa na mifumo
mingine kama ya ankara, mauzo na stakabadhi kwa kufanya mabadiliko
machache na una ruhusu matumizi ya fedha mbalimbali.
Aliongeza kuwa mfumo huo ni wa uwazi kwa sababu ukomo wa kila risiti
unahakikiwa na una uwezo wa kutambua huduma kama imetolewa au la.
Kuhusu kodi ya zuio iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2013, kamishna huyo
alisema imekuwa na changamoto kwa idara na taasisi za serikali kutokana
na wahusika kukosa uelewa wa kutosha wa utozaji wa kodi husika.
“Kumekuwa na mkanganyiko kati ya utozaji wa kodi ya zuio ya asilimia
mbili katika usambazaji wa bidhaa kwa Idara na taasisi za serikali
zinazotegemea bajeti ya serikali kuu kwa asilimia 100 na ile ya asilimia
tano kwa huduma,” alisema.
Alisema kupitia mafunzo hayo washiriki wataelimishwa kuhusu mabadiliko
ya sheria fedha ya mwaka 2016, sheria ya kodi ya ongezeko la thamani ya
mwaka 2014, kodi ya zuio katika bidhaa na huduma na mfumo huo wa
ukusanyaji maduhuli.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi TRA, Richard Kayombo,
alisema utumiaji wa risiti za kawaida umekuwa ukitoa mianya ya upoteaji
wa mapato hivyo kupitia mafunzo hayo wanaamini washiriki watatambua
wajibu wao katika kuhakikisha makusanyo yanaongezeka.
Mhasibu Mwandamizi kutoka Bodi ya Sukari Tanzania, Devotha Sanga,
alitaja changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni kushindwa kutambua viwango
vinavyotakiwa kutozwa kwa mtu binafsi au kampuni kupitia kodi ya zuio
ni asilimia ngapi.
Pia alisema katika kodi ya ongezeko la thamani kumekuwa na changamoto ya risiti za kughushi ambazo wanashindwa kuzitambua.
Tags
TRA