MFUGAJI mmoja wilayani Kalambo katika mkoa wa Rukwa amegoma kumrejesha
kwa ndugu zake kijana ambaye iliaminika amekufa kwa kuliwa na fisi,
lakini akakutwa akichunga mifugo; akidai kwanza malipo ya sh. milioni
moja alizotoa kwenye msiba wake.
Tukio hilo la kushangaza lilitokea mwishoni mwa wiki baada ya kijana
huyo kukutwa akichunga ng'ombe wa Juma Maeka, ambaye aligoma kumrejesha
kwa ndugu zake akitaka kwanza kulipwa sh. milioni moja.
Mkazi wa kijiji cha Tunyi kata ya Mabwekoswe wilayani Kalambo mkoani
Lukwa, Mtipa Sisunzu (20) alipotea Septemba, mwaka jana katika mazingira
ya kutatanisha na ndugu zake waliweka msiba wakiamini alikufa kwa
kuliwa na fisi.
Lakini Sisunzu alizua taharuki kijijini hapo wiki iliyopita baada ya
kukutwa akichunga ng'ombe wa Maeka, hali iliyopelekea ndugu kushikwa na
butwaa.
Diwani wa kata hiyo, Julias Siwale alisema kabla ya kupotea, kijana huyo
alikuwa akifanya kazi ya kuchunga ng’ombe wa mfugaji huyo.
Baada ya kupotea kwake na kuwapo kwa msiba nyumbani kwao, alisema
Siwale, Maeka alitoa sh. milioni moja kwa ajili ya kusaidia msibani.
Alisema baada ya msiba kumalizika, kila mtu aliamini kuwa kijana huyo alikuwa amefariki dunia.
Lakini wanakijiji walikuja kushangaa baada ya ndugu wa kijana huyo
kumkuta akichunga ng’ombe wa mfugaji huyo katika moja ya mbuga zilizopo
mbali na kijiji hicho.
Alisema baada ya kumtaka warudi nae nyumbani, Maeka aliwakatalia akitaka
kulipwa fedha ambazo alitoa wakati wa msiba na kupelekea kujitokeza kwa
malumbano baina yao.
Diwani Siwale alisema baada ya malumbano kuwa makubwa, ikawalazimu kama
uongozi wa kata kuingilia kati na kumwamuru mfugaji huyo kumrejesha
kijana huyo kwa ndugu zake sambamba na kumpiga faini ya sh. 100,000 kama
fidia usumbufu aliowapa ndugu wa kijana huyo.
Mtendaji wa kata hiyo, Oswald Kalindo alisema awali kila mtu aliamini
kijana huyo alikuwa amefariki dunia kwa kuliwa na fisi kwani walimtafuta
kila kona ya kijiji na maeneo mengine kwa muda mrefu bila mafanikio.
Alisema kupatikana kwa kijana huyo kumeleta faraja kwa wakazi wa kata
hiyo kutokana na kwamba kila mmoja alikuwa na shaka juu ya kupotea
kwake.
Alisema wanajipanga kuitisha mkutano kuzungumzia suala hilo.
"Wananchi wametuomba viongozi tuitishe mkutano mkuu ili waweze
kuzungumzia hali hii wakidai huenda kuna vijana wengi waliodaiwa kufa
wakawa hai wakifanyishwa kazi za kuchunga ng'ombe au kulima mashamba,"
alisema Kalindu.
Tags
MAAJABU
