Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Dkt. Abdalla Juma Saadala” Mabodi” akitoa ufafanuzi wa mabadiliko ya
Katiba ya CCM yaliyofanyika mwaka 2017, kwa washiriki wa mafunzo elekezi
ya kuwajengea uwezo ili waweze kuzikabili changamoto za uchaguzi wa
chama na jumuiya zake.
Mwasilishaji ambaye pia ni Afisa
kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma, Nd.Alhaji Rajab Kundya akiwasilisha
mada za Mabadiliko ya katiba ya CCM ya mwaka 2017, pamoja na maboresho
ya kanuzi ya uchaguzi ya chama hicho.
Ni baadhi ya washiriki wa mafunzo
hayo wakifuatilia kwa makini mada zinazowasilishwa wakiwemo makatibu,
wenyeviti , wajumbe wa kamati za siasa za ngazi za matawi hadi majimbo
kwa chama na jumuiya zake, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkoa wa Mjini
Amani Unguja.(PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR).
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WAFUASI wa CCM wameshauriwa
kutowachagua baadhi ya wanachama wenye kashfa na tabia za usaliti kuwa
viongozi wa ngazi mbali mbali zinazowaniwa ndani ya chama na jumuiya
zake hicho kupitia uchaguzi unaoendelea hivi sasa.
Ushauri huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “
Mabodi” katika mwendelezo wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo
watendaji na viongozi wa majimbo ya Mkoa wa Magharibi Unguja, ili
waelewe kwa kina Mabadiliko ya Katiba ya CCM na kanuni mbali mbali
yaliyofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Dkt. Mabodi alisema chama hicho
ili kiendelee kuimarika ni lazima wanachama wake ambao ni waaminifu
wafanye maamuzi magumu ya kuwaweka kando kwa njia ya Kidemokrasia baadhi
ya wanachama wenye dalili na sifa za usaliti sambamba na kamati za
maadili kuanzia ngazi za chini kuwafanyia vikao vya kikanuni kuwajadili
na kuwapatia fursa za kujitetea endapo watakutwa na makosa wachukuliwe
hatua kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba na kanuzi za maadili.
Pia Dkt. Mabodi alieleza kwamba
lengo la kuchukua maamuzi hayo sio kuwaonea watu hao bali ni kukisafisha
chama ili kibaki na wanachama waadilifu watakaokilinda na kukipigania
katika mazingira yoyote hasa wakati wa chaguzi za chama na dola pamoja
na vipindi mbali mbali vya misukosuko ya kisiasa nchini.
“ Kama tunahitaji kufanya
matengenezo ndani ya nyumba yetu ni lazima nyufa zilizomo zote tuzibomoe
na kuanza kujenda upya awamu kwa awamu kwa nia ya kupata nyumba imara
na ya kudumu, na uko ndiko tunakoelekea kwa sasa lazima tupate makada
wa kweli wanaotamka dhana ya Mapinduzi daima pamoja na kuulinda muungano
kwa vitendo na sio kauli pekee.”, alisema Dkt. Mabodi.
Akizungumzia mabadiliko ya Katiba
ya CCM yaliyofanyika hivi karibuni, alisema yamelenga kuongeza ufanisi
ndani ya chama hicho kwa kupunguza idadi za viongozi na vikao
vilivyokuwa vikitumia fedha nyingi kwa uendeshaji wake na kubaki na
mambo machache yatakayoongeza ufanisi kwa matumizi mazuri ya rasilimali
za chama na kiutendaji.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaagiza
washiriki wa Mafunzo hayo kuwa mabalozi na walimu wa kuwaelekeza kwa
ufasaha wanachama wa CCM ambao hawakupata fursa hiyo ili nao wajue lengo
la mabadiliko.
Hata hivyo aliupongeza Mkoa huo
kwa kazi nzuri walioyofanya katika Chaguzi za Dola za Octoba 2015 na
Machi, 2016 kuwa zilizaa matunda ya kupatikana kwa Serikali ya Awamu ya
Saba chini ya Uongozi wa Dkt. Shein pamoja na viongozi wengine wakiwemo
Madiwani, Wawakilishi na Wabunge licha ya kuwepo kwa changamoto nyingi
za kisiasa.
Aidha aliweka wazi kwamba
suala la kuimarisha uchumi wa chama hicho kupitia miradi ya ndani ya
chama kuanzia ngazi za matawi hadi taifac halina mbadala kwani linagusa
moja kwa moja maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa.
Akijibu hoja za baadhi ya
washiriki wa mafunzo hayo mwasilishaji wa mada ya mabadiliko ya Katiba
ya chama hicho, Alhaji Rajab Kundiya alieleza kwamba ndani ya maboresho
ya kanuni ya uchaguzi haijamzui mfanyakazi wa umma kutowania nafasi
yoyote ya uongozi ndani ya CCM, isipokuwa wafanyakazi wenyewe wana
miongozo na taratibu zao za kiutumishi katika sehemu zao za kazi.
Sambamba na hayo alisema kupitia
marekebisho ya kanuzi za uchaguzi na maadili zimeweka utaratibu mzuri
utakaomaliza tabia za kupanga safu na rushwa ndani ya chama hivyo kutoa
fursa kwa wapiga kura kumchangua kiongozi anayefaa na mwenye sifa
zinazokubalika katika michakato ya kidemokrasia na kiuongozi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Magharibi, Nd. Yussuf Mohamed Yussuf alisema washiriki hao ni wadau
wakubwa wa masuala ya chaguzi za chama na dola hivyo wanatakiwa kutumia
mafunzo hayo kuongeza uzalendo, uaminifu na umakini zaidi katika
uchaguzi huo.
Tags
CCM