
Mzozo mpya umeibuka kati ya tume huru ya uchaguzi nchini Kenya, na
vinara wa mrengo wa upinzani wa NASA kuhusu utangazaji wa matokeo rasmi
ya kura za Urais.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ‘IEBC’ imeijibu mrengo wa upinzani wa
NASA kufuatia vitisho vyake vya kususia uchaguzi iwapo tume hiyo
itafaulu kwenye rufaa iliyowasilisha mahakamani dhidi ya uamuzi wa
mahakama ulioruhusu matokeo ya kura za Urais kutangazwa katika kituo cha
kupigia kura.
Hii ni baada ya viongozi wa upinzani kuishauri IEBC dhidi ya kusaka njia
za kubadili mipango hiyo ili kutangaza matokeo ya kura za Urais katika
kituo cha kitaifa jinsi ilivyokuwa matokeo ya miaka iliyopita.
Tume hiyo kupita mwenyekiti wake Wafula Chebukati, imeeleza kuwa
haitobadili msimamo wake wa kukata rufaa na kuwaambia viongozi wa
upinzani kuheshimu mahakama na kutumia njia za kisheria kutatua
malalamiko yao.
Viongozi wa mrengo wa upinzani wakiongozwa na Mgombea wa Urais, Raila
Odinga, walitishia kususia uchaguzi iwapo tume hiyo itakata rufaa na
kuruhusu matokeo ya Urais kutoka kila kituo kutangazwa kitaifa.
Taifa la Kenya linatarajiwa kuandaa uchaguzi mkuu wa Urais baadaye mwaka
huu huku ushindani mkali ukitarajiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta
anayewania kiti hicho kupitia mrengo wake wa Jubilee na Raila Odinga,
anayebeba bendera ya mrengo wa Upinzani wa NASA.
Tags
Kenya