
Nilishangaa sana baada ya kusoma ujumbe wa Zitto akidai anajuta kuzaliwa
Tanzania kwa sababu wabunge hawakumchagua Lawrence Masha kuwa Mbunge wa
EALA.
Zitto amesahau kuwa miaka tisa iliyopita alimtuhumu Masha akiwa Waziri
wa Mambo ya Ndani kuwa anapanga mkakati wa kumfilisi Mzee Reginald Mengi
kwa sababu Media zake zilikuwa zinaandika habari za kupinga ufisadi.
Zitto huyu huyu leo eti anajuta kwa nini wabunge hawakumchagua Masha kuwa Mbunge.
Wanasiasa wa Tanzania ni viumbe wa ajabu kweli.
Ninaambatanisha maneno ya Zitto aliyoyasema mwaka 2008 kuhusu Lawrence Masha.
Zitto apasua jina la waziri kijana.
2008-12-07 13:37:18
Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema ana ushahidi kuwa,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha ndiye aliyepeleka hoja
ya kumhujumu Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi katika vikao vya juu na
kwamba taarifa hizo alithibitisha kuzipata jana.
Akiongea na Nipashe Jumapili jana, Zitto alisema waziri huyo, kwa
taarifa alizonazo za kuaminika, alitoa hoja kuwa vyombo vya habari vya
IPP vimekuwa mstari wa mbele kupiga vita ufisadi na hii inailetea
matatizo serikali.
Hivyo, aliomba serikali ipange mikakati ya kumfilisi Mengi, kitendo
ambacho kitasababisha kudhoofishwa kwa vyombo vyake vya habari ambavyo
vitashindwa kuendelea kuupinga ufisadi.
Zitto alisema yeye hana sababu ya kumtetea Mengi ila hawezi kunyamaza
kuona Mtanzania anayeipenda nchi yake na kulazimika kupinga ufisadi
anafanyiwa hujuma.
Aidha, Zitto aliliambia Nipashe Jumapili kwamba, vyombo vya habari
vimekuwa mstari wa mbele kuanika maovu ya ufisadi na vyombo hivyo lazima
vilindwe na Watanzania wote wazalendo.
Akijibu hoja ya Mengi iliyotolewa jana kuwa yupo tayari kutupwa jela
ikithibitishwa kuwa amedanganya na kumwomba Masha pia aseme kama atakuwa
tayari kujiuzulu iwapo ukweli wa maneno ya Mengi yatathibitishwa, Masha
aliliambia Nipashe Jumapili kuwa hawezi kujiuzulu kwa sababu nia yake
ya kuwaagiza polisi kufanya uchunguzi ni kumlinda Mengi.
Alisema kutokana na taarifa ambayo Mengi aliipeleka kituo cha polisi cha
Oysterbay, polisi wameamua kuifanyia uchunguzi ili kuhakikisha maisha
yake yanakuwa salama.
``Nia ya serikali ya kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Mengi ni
kuhakikisha kuwa tunamlinda,`` alisema Masha na kuongeza kuwa hana
tatizo na maneno yaliyotolewa na Zitto ili mradi awe na ushahidi.
Amesema, hata kama hawamuamini, basi waupeleke huo ushahidi kwa Rais au
Waziri Mkuu kuuonyesha na kama ikibainika kama ni kweli yeye ndiye
anayemhujumu Mengi, basi atajiuzulu.
Akasema kuwa yeye hakusema kuwa atamshughulikia Mengi kama
alivyonukuliwa kwenye baadhi ya magazeti ila alisema kuwa sheria
itachukua mkondo wake kama ikibainika kuwa tuhuma zilizotolewa ni za
kweli.
Akiongea na TBC1 juzi, waziri Masha, alisema kuwa kama Mengi ana
ushahidi wa tuhuma alizotoa, serikali haitapata shida ya kuhangaika na
ushahidi na imemtaka apeleke ushahidi huo.
Kuibuka kwa sakata hilo kunatokana na Mengi kumtuhumu waziri mmoja kuwa
ameagiza abambikiwe kodi bandia ya kiasi kikubwa atakachoshindwa kulipa
ili hatimaye afilisiwe.
Alimtuhumu waziri huyo kuwa amekuwa akimtumia ujumbe wa vitisho kutokana
na vyombo vyake vya habari kuwa mstari wa mbele katika kupigia kelele
ufisadi.
Akifungua kongamano la kuwajengea uwezo vijana wa Chama Cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa vijana
wa chama hicho, John Mnyika, aliwataka vijana kuendeleza vita ya ufisadi
na kutokatishwa tamaa na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya watu.
Aliwakumbusha vijana kuwa ni wajibu wao kupigania haki zao kwa manufaa
ya taifa na kwamba wanapaswa kukosoana pindi mwenzao anapofanya vibaya.
``Kwa maoni yangu naona kama kauli ya Masha ya kumtaka Mengi awasilishe
ushahidi ndani ya siku saba ni ya kukurupuka kwa kuwa mbona
nilipotuhumiwa na Mtikila kwamba nimeshiriki kumuua Chacha Wangwe
hakusema lolote hadi leo?
Tunashangazwa sana na kauli ya Masha, tulidhani labda angechunguza
kwanza kabla hajazungumza na katika hili nawaomba vijana muwe makini na
vijana kama hawa na muwakosoe waziwazi,`` alisema.
Alionya kuwa iwapo vijana hawatakosoana jamii itapoteza imani juu ya
utendaji wao na kuondoa matumaini ya taifa kuhusu umuhimu wa vijana.
Hata hivyo,alisema vita dhidi ya ufisadi bado ni kubwa kwa kuwa ni asilimia 10 tu imetekelezwa.
``Msibweteke na ushindi huu, ufisadi unaozungumziwa ni wa utawala wa
Mkapa, katika awamu ya nne kuna ufisadi kama wa Richmond na Buzwagi kwa
hiyo tunapaswa kupambana zaidi,`` alisema.
SOURCE: Nipashe
Tags
Zitto Kabwe