
Zuio la kusafirisha mchanga wa madini kwenda nje ya nchi liliwagawa
wabunge katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya
Nishati na Madini uliofanyika wiki hii.
Licha ya wabunge wengi kukubali kwamba Taifa halinufaiki ipasavyo
kutokana na uchimbaji wa madini pamoja na rasilimali nyingine
zinazoendelea kuvunwa nchini, baadhi ya wabunge, hasa wa upinzani,
hawakubaliani na namna mchakato mzima unavyoendeshwa.
Hoja inayotolewa na wapinzani ni ubovu wa sera, sheria na mikataba yote
ya madini ambayo mingi haijawekwa wazi hivyo kutolinufaisha Taifa kwa
kiasi kilichotarajiwa.
Wapinzani wanataka mchakato wa kufanya marekebisho yoyote uanzie katika
mikataba badala ya mchanga ambao ni sehemu ndogo ya kinachopotea.
Akichangia hoja, mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa alisema agizo la Serikali linaweza likawa na athari kwa
wawekezaji wa sekta ya madini ambao mitaji yao imeelekezwa huko.
Alikumbusha kwamba wizi wa madini ulielezwa siku nyingi hata ripoti ya
baadhi ya tume zilizoundwa zilibainisha mapungufu yaliyomo na kushauri
yaliyoelezwa ndiyo yanapaswa kupewa kipaumbele katika mapambano haya.
Mwita Waitara, mbunge wa Ukonga (Chadema), alisema tatizo lililopo ni
mikataba ya madini ambayo haijawahi kupelekwa bungeni ili wawakilishi
hao wa wananchi waione na kutafuta namna sahihi ya kurekebisha kasoro
zilizopo.
Alisema licha ya Rais kuunda kamati ya kuchunguza na wabunge wengi
kuguswa na wizi wa madini, bado mjadala unaoendelea unakosa uhalisia kwa
sababu kila mmoja anatoa hoja bila kujua mkataba una vifungu vipi
vinavyotekelezwa. Alisema kwa kuwa mikataba ilipitishwa na chama tawala
ambacho leo kimegundua kuibiwa, “wabunge wanahitaji kuiona mikataba hiyo
na kujua mambo mliyokubaliana.”
Wakati wabunge hao wakipendekeza hayo, Waziri Kivuli wa Nishati na
Madini, John Mnyika alisema mwisho wa siku atakayepoteza kwenye vita
hivi ni Serikali ambayo italazimika kuilipa Kampuni ya Acacia
inayosafirisha mchanga huo fidia kutokana na hasara itakayopata kwa muda
wote wa zuio.
Wabunge wengi wa chama tawala wanamuunga mkono Rais kwa hatua hiyo,
wakisema ni namna sahihi ya kwenda kwenye mabadiliko ya mikataba
iliyosainiwa siku nyingi na wawekezaji waliopo.
Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema hata kama
watakaoathirika na agizo hilo wataenda mahakamani na Serikali ikawa na
uhakika wa wizi huo, itashinda kwa kuwa suala hilo halikuwa sehemu ya
mkataba.
“Hawatafanya chochote tukiwa na ushahidi. Tume ya kwanza imeonyesha
udanganyifu ambao ni kinyume na masharti ya mkataba. Hata wakienda
popote tutawashinda. Nampongeza Rais kwa anachokifanya,” alisema.
Msimamo wa Mapunda unafanana na wa Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab
ambaye alisema mchakato huo unapaswa kuendelea kwani hakuna
kitakachoitisha Serikali.
“Tukiwa na ushahidi, hata tukishtakiwa tutaenda kutoa argument.
Tunaibiwa, huo ni ukweli, tunaweza kubishana kwenye kiwango tu,” alisema
ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Wabunge kutoka maeneo yenye migodi walitoa ushahidi wa wizi unaofanywa.
Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige alisema suala hilo lilikuwapo
anakotoka kiasi cha kuwashawishi wananchi kuyavamia malori yaliyokuwa
yanasafirisha mchanga huo na kuuiba.
“Walipochenjua kwa njia za kienyeji, kiroba cha kilo 50 cha mchanga
kilitoa mpaka Sh50 milioni. Sasa hivi ulinzi umeimarishwa, malori hayo
yanasindikizwa na askari wenye silaha,” alisema Maige ambaye ni mtaalamu
wa biashara.
Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Msukuma aliwataka wabunge wenzake, bila
kujali itikadi kuungana kwenye vita hii kwani jamii zinazozunguka migodi
zinafahamu athari za kudumu za wawekezaji wa sekta hii.
“Wametuachia mashimo makubwa. Njooni muyaone. Wameondoka na kila kitu
wakati wananchi wanaozungua bado ni masikini na hawana huduma za uhakika
za jamii,” alisema Musukuma.
Aliwananga wanaopinga hasa Chadema kwamba wanawatetea wezi hao wa madini
ambao kamati imeanika wanachokifanya kwakuwa wamepokea fedha ili
wafanye hivyo na wanachokisema kinawaondolea uzalendo mbele ya jamii.
“Nawafahamu waliopewa fedha. Niwataje…niwataje! Semeni basi. Tunajua kuwa mna-retire imprest mlizolipwa,” alisisitiza Musukuma.
Ni suala lililomgusa hata Spika wa Bunge, Job Ndugai aliyesema Bunge
lake linaunga mkono hatua alizochukua Rais kukabiliana na jambo hilo
kubwa ambalo halifai kufumbiwa macho na akataka kupuuzwa kwa
wanaowatetea wezi wa madini. “Hatuwezi kuwa tunaibiwa halafu tunacheka
cheka. Hii ni vita kubwa ingawa wapo wat wanaotetea. Unakuta ni mbunge
anayetoka sehemu yenye upungufu wa madawati, dawa hospitalini na
barabara mbovu. Hii ndiyo namna ya kuwatambua. Mngejuaje sasa? alisema
Ndugai akiahirisha kikao cha Bunge Ijumaa.
Tags
mchanga wa madini