
Mwanamume aliyefahamika kwa jina la Luhende Lusangija (34) mkazi wa
Mwinamila Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga amekutwa amejinyonga
nyumbani kwake kutokana na kile kilichotajwa kuwa mke wake alikuwa
anauza mali za familia kutokana na mikopo aliyokuwa anadaiwa.
Tukio hilo limetokea Jumamosi Juni 3,2017 majira ya saa 11 alfajiri
ambapo marehemu akiwa na watoto wake watatu nyumbani, aliamka na kisha
kuchukua mtandio huku watoto wake wakiwa wamelala, na kuamua kujitundika
kitanzi sebuleni, na kusababisha kifo chake papo hapo.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Mwanamume huyo amejiua kutokana na kile
kinachodaiwa kuwa ni ugomvi wa siku nyingi na mke wake ambaye siku
kabla ya tukio alikuwa ameshaukimbia mji wake.
Wakisimulia tukio hilo majirani zake Safina Javali, alisema marehemu
alikuwa na ugomvi na mkewe muda mrefu ambapo kila siku walikuwa
wakipigana, kwa madai kuwa mwanamke alikuwa akikopa mikopo, na baada ya
kushindwa kuirejesha alikuwa akiuza vitu vya ndani wakati mumewe akiwa
safarini kwenye majukumu yake ya kikazi.
"Juzi alipokuja mwanamume kutoka safarini akakuta kitanda kimefungwa
kwenda kuuzwa, ili mwanamke alipe deni la mikopo aliyokuwa akiichukua,
ndipo ugomvi mkubwa ulipozuka hadi kusababisha mwanamke kuukimbia mji
wake na kwenda kusiko julikana", alisema Javali.
Akiongea kuwa baada ya tukio hilo kutokea walimsikia mtoto wake wa miaka
7 majira ya saa moja asubuhi akilia kwa uchungu na kupiga kelele, kuwa
baba yake amekufa kwa kujinyonga na walipofika kwenye nyumba na
kuchungulia mlangoni ndipo wakamuona amening'inia kwenye paa la sebuleni
akiwa ameshafariki.
Naye mwenye nyumba Halima Issa ambapo marehemu alikuwa mpangaji wake,
alisema mji huo ulikuwa na ugomvi mara kwa mara na walikuwa
wakiwasuluhisha lakini ugomvi wao ulikuwa pale pale, na walipopata
taarifa ya kifo chake walifika eneo la tukio kisha kuwasiliana na
uongozi wa mtaa ili kufuata taratibu za kisheria.
Aidha Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mwinamila Ngokolo mjini Shinyanga Yohana
Munisa, alikiri kupokea taarifa za marehemu huyo majira ya saa moja
asubuhi, na alipofika eneo la tukio alimkuta Lusangija akiwa tayari
amejinyonga, ndipo akatoa taarifa polisi ambapo nao wakafika ili
kuuchukua mwili wa marehemu.
Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Elias
Mwita alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya
rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, huku ndugu wa marehemu wakitafutwa ili
kuuchukua mwili huo kwa taratibu za mazishi.
Tags
kujinyonga