KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, imeendelea kufanya kweli kwenye kambi yake nchini
Uganda baada ya muda mchache uliopita kuichapa URA mabao 2-0.
Mchezo wa huo wa kimataifa wa
kirafiki ulifanyika Uwanja wa Phillip Omondi, ambapo Azam FC imeutumia
kama maandalizi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL).
Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica
Cioaba, alichezesha kikosi kingine cha pili katika mchezo huo na
kuwapumzisha wachezaji walioanza kwenye mechi mbili zilizopita.
Mabao yote mawili ya Azam FC
yamefungwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, moja katika kila kipindi cha
mchezo huo, la kwanza akifunga dakika ya 19 kwa shuti kali nje ya eneo
la 18 kabla ya kutupia jingine la aina hiyo dakika ya 47.
Licha ya mabadiliko makubwa
kikosini kwenye mchezo huo, bado timu hiyo ilionekana kucheza na kuwa
imara kwenye eneo la ulinzi huku kipa Mwadini Ally, akifanya kazi kubwa
baada ya kuokoa michomo mingi ya URA.
Mara baada ya mchezo huo wa tatu
wa kirafiki kwenye kambi ya timu hiyo nchini Uganda ambapo jana ikitoka
sare ya bao 1-1 na mabingwa wa Uganda KCCA, Azam FC itashuka tena
dimbani Jumapili ijayo kumenyana na Onduparaka, mtanange utakaofanyika
Uwanja wa Nambole kuanzia saa 10.00 jioni.
Ziara hiyo itahitimishwa Jumatatu
ijayo kwa Azam FC kucheza mchezo wa tano wa kirafiki dhidi ya washindi
wa tatu wa Ligi Kuu Uganda msimu uliopita, Vipers FC, utakaofanyika
Uwanja wa St Marys uliopo Kitende, Uganda.
Kikosi cha Azam FC leo:
Mwadini Ally, Swaleh Abdallah,
Hamimu Karim, Abdallah Kheri, David Mwantika (C), Stephan Kingue, Idd
Kipagwile/Braison Raphael dk 57, Salmin Hoza/Frank Domayo dk 84, Yahaya
Mohammed/Yahya Zayd dk 70, Enock Atta/Masoud Abdallah dk 55, Joseph
Mahundi/Ramadhan Singano dk 81
Tags
Azam fc