BANDA MEDIA BLOG

No title

 




DKT KIJAZI AWATAKA MAAFISA HABARI WA SERIKALI KUTOA ELIMU YA SENSA YA MAKAZI


 Na Munir Shemweta, WANMM TANGA

KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi amewataka maafisa Habari  na Mawasiliano Serikalini kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika Agosti mwaka huu. 

Dkt Kijazi amesema hayo mkoani Tanga leo wakati akiwasilisha mada kuhusiana na Sensa ya Makazi  kwenye kikao cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kinachoendelea mkoani Tanga.


"Ninyi Maafisa Habari mnatakiwa kuelimisha wananchi umuhimu wa taarifa za majengo, na ni kwanini ifanyike wakati huu" alisema Dkt Kijazi.

 Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ni vizuri Maafisa Habari wakashiriki vyema katika zoezi hilo kwa kutoa elimu sambamba na kubainisha changamoto na kutoa mrejesho hata kabla ya kuanza kwa sensa ya makazi. 

DKt Kijazi amesema, takwimu zitakazopatikana wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi zitaisadia serikali kupanga na kutekeleza mipango yake itakayoleta mabadiliko katika maendeleo ya kiuchumi.

 " Naomba nitoe rai kwa wananchi, waiamini serikali yao kwa kuwa zoezi hili la sensa ya watu na makazi litaiwezesha serikali kupanga kutekeleza mipango ya maendeleo itakayoleta mabadiliko katika uchumi vinginevyo hatutapata takwimu sahihi" alisema Dkt Kijazi. 

Aidha, alieleza kuwa, lengo la sensa ya watu na makazi pia ni kuiwezesha serikali  kuwa na benki ya taarifa za makazi sambamba na kuhakikisha inakuwa na mikakati ya kujua makazi na kujua miji na  vifaa vilivyotumika. 

"Kama nchi lazima tuzingatia mikakati kulingana na takwimu zilizopo na hii ni Sensa ya kwanza ya makazi" alisema Dkt Kijazi. 


Kwa upande wake Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 Anna Makinda amesema, upo mkakati wa elimu na uhamasishaji kuhusiana na sensa na Maafisa Habari wa Serikali wanalo jukumu la kuhamasisha umuhimu wa sensa. 

 "Kila aliyekuwa serikalini lazima azungumzie sensa na maafisa habari ndiyo wenyewe na mkasaidie kuhamasisha hasa katika mitandao ya kijamii  kwa kuwa wanaosoma zaidi mitandao ni vijana" alisema Makinda.

-----------MWISHO-----------------



 

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG