WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WANAFUNZI WALIORUDISHWA NCHI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wanafunzi waliokuwa wanasoma katika vyuo mbalimbali nje ya nchi ambao walirudishwa nchini kufuatia kuzuka kwa janga la UVIKO19 pamoja na kuibuka kwa vita kati ya Urusi na Ukraine wawasilishe taarifa zao Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Mei 12, 2022) wakati
akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafuwe katika kipindi cha maswali ya
papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka
kujua Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi hao kuendelea na
masomo wakiwa hapa nchini.
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikishia
wanafunzi hao wanasaidiwa kumaliza masomo yao wakiwa hapa nchini, Serikali
inawataka wawasilishe taarifa zao TCU ambayo imeweka utaratibu unaoruhusu
wanafunzi hao kuhamisha viwango vya ufaulu wa masomo vitakavyowawezesha
kuendelea na masomo yao nchini.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kununua
viuadudu kwa ajili ya kupuliza katika maeneo mbalimbali na kutokomeza mazalia
na mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria. Dawa hizo zinatengenezwa
na kiwanda cha Kibaha Tanzania Biotech Product Limited.
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo wakati
akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Tweve ambaye
amesema Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa wa katika kujenga kiwanda cha
viuadudu kwa gharama ya wastani wa bilioni 46.
“Wizara ya Afya iliingia mkataba wa kununua dawa
hizo na haikufanya kama ilivyokubalika. Je Serikali haioni umuhimu
wa kuingia mkataba mpya na kiwanda hiki ili kuweza kununua dawa zitakazo saidia
kutokomeza malaria nchini?” amehoji.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kwamba suala la
ukarabati wa miundombinu mbalimbali katika shule kongwe nchini ni endelevu na
kila mwaka Serikali inatenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu
swali la Mbunge wa jimbo la Mwanga, Anania Thadayo aliyetaka kufahamu Serikali
ina mpango gani wa dharura wa kuzifanyia ukarabati shule nyingi ambazo
ilizozijenga kwa kipindi kirefu huku baadhi yake zimeanza kuchakaa.
