MARUFUKU MAFUTA YA UBUYU ITAZAMWE UPYA

Adeladius
Makwega-TANGA
Mwishoni
mwa wiki nilikuwa najiandaa na safari ya kwenda Tanga, nilipokuwa natafuta
zawadi za kwenda nazo huko kwa ajili ya familia yangu, nilibaini kuwa japokuwa
Tanga wana matunda mengi lakini ubuyu haupo. Kwa hiyo nilimuagiza kijana mmoja
wa Chigogo aniletee gunia la ubuyu ili kuweza kwenda nao huko.
Kweli
nililetewa gunia zima la ubuyu kwa shilingi 15,000/-huku likiwa limeja pomoni, nikaliangalia
vizuri lile gunia nikasema ni mzigo mkubwa mno kusafiri nao hadi Tanga.
Nikafikiriii nikaenda mashine jirani na kuwaeleza waupitishe katika mashine ya
kukoboa ili nipate unga wake tu na mzigo uwe mwepesi.
Nilifanya
hivyo na kupata madebe mawili ya unga wa ubuyu, alipomaliza kazi hiyo nikaona
mbegu za ubuyu nyingi katika madebe zaidi ya manne. Nikauliza, sasa hizi mbegu zinatupwa?

Kijana
wa mashine akajibu, ndiyo, zinatupwa mzee, lakini zamani tulikuwa tunazikamua
mafuta au tunasaga katika jiwe/kinu na kuwa kiungo kizuri sana kwa mboga za
Wagogo na wengine wakifanya baishara ya unga huo wa mbegu za ubuyu na mafuta
yake.
“Kwa
bahati mbaya Serikali ikapiga marufuku, wakisema mafuta ya ubuyu yana madhara
kiafya.”
Nikamwambia
kijana wa mashine nifungie mbegu zangu, nikawekewa katika kiroba na kwenda nazo
kwangu. Kijana aliyebeba akauliza mzee hizi unakwenda nazo wapi? nikamwambia
nyumbani kwangu kuna bonde kwa hiyo hizi mbegu naenda kuzimwaga hapo kupunguza mmomonyoko
wa udongo katika bonde hilo.
“Mzee
zitaota hizi, maana ardhi ya Dodoma ni udongo wa mibuyu.”

Nikajibu
kuwa ikiwa inaota nitakuwa naipunguza kidogo kidogo.
Mzee,
hizi mbegu zamani ilikuwa pesa ya maana sana, hata jirani yako alikuwa ni
miongoni wa wafanyabiashara wa mafuta ya ubuyu, alisema kijana huyu.

“Mbegu
za ubuyu kwa Dodoma, Singida na mikoa mingi jirani zinapatikana kwa wingi kama
zingetumika sana zingeua kabisa soko la mafuta ya madukani na sisi Wagogo ni
kiungo chetu cha miaka mingi hasa hasa zile mbegu zikitwangwa katika kinu na
kuungia mboga zetu, mboga inanoga sana.”
Aliniambia
kijana aliyenibebea mizigo, huku nikimtambua kwa jina moja la Josefu.
Nikashushiwa
mizigo yangu na kwenda hadi kwa jirani, Nilipiga hodi na kukaribishwa vizuri,
nikamuuliza eti jirani uliwahi kufanya biashara ya mafuta ya ubuyu?
Mama
huyu anayefahamika kama Mdala Zipora alinijibu kuwa mwanangu biashara hiyo
ilishamiri mno wakati wa Urais wa Jakaya Kikwete na lita moja ya mafuta ya
ubuyu yalikuwa kati ya shilingi 20,000-30,000/-
Hivi
sasa kuna shida ya mafuta, mimi wala nisingepata tabu, ningekusanya mbegu zangu
na kukamua mafuta hayo, ningepata pesa na ningepata mafuta ya kupikia. Alisema
jirani yangu huyu ambaye ni mama mwenye umri kati ya miaka 63-65.
Binafsi
nikasema kama kwa mwaka 2013 lita moja iliuzwa shlingi 30,000/- miaka 10 sasa
lita moja ingefika zaidi ya shilingi 50,000/- ambayo ni mara 16 ya lita ya petrol
kwa bei ya sasa na pia ni mara tano ya bei ya lita moja ya asali ya nyuki
wakubwa kwa sasa inayouzwa shilingi 10,000/-

Msomaji
wangu hiyo nakisi ya bei ya lita moja ya mafuta ya ubuyu kwa lita moja asali au
petrol inakupa picha ya thamani ya mafuta hayo.
Lakini
Serikali Ikatangaza mafuta hayo yana madhara kiafya hivyo yasitumike kabisa.
“Hapa
Dodoma palikuwa na Mkorea ambaye alikuwa akinunua unga wa ubuyu na mbegu zake
ambazo alizikamua na kuyachukua mafuta hayo na mimi nilikuwa naenda kukamua na
kuyauza kwa wateja wangu wengi yaani baba! Hata ukikamua robo ya lita unauza kwa
shilingi kati ya 6,000-7,000/-.” Alisema Mdala Zipora.
Kwa kuwa
Jakaya Kikwete alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kati ya mwaka
2005-2015,binafsi nikaanza kutafuta taarifa za mafuta ya ubuyu katika kipindi
hicho juu ya katazo hilo na athari zake kiafya.
Kulingana
na taarifa iliyoandikwa na mwanahabari Theopista Nsanzungwako ya Julai 8, 2013
katika gazeti la serikali Habari Leo ilisema kuwa,

“Hivi
karibuni kumekuwa na wimbi la Wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu kama dawa,
na kuwaelekeza wananchi kunywa, napenda kuwataarifu kuwa mafuta hayo ni hatari
kwani yana tindikali ya mafuta.”
Gazeti
hilo lilimnukuu msemaji wa TFDA Gaudensia Simwanza aliyekuwepo katika maonesho
ya 37 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam huku msako ulifanyika katika
maonesho hayo kwa wale waliodiriki kufanya biashara hiyo hapo kiwanjani.
Jambo
hilo halikuishia hapo nalo Gazeti la Mwananchi la Julai 31, 2013, siku 23 baada
ya TFDA kusema hayo, lilimnukuu Mkemia Mkuu wa Serikali wakati huo, Profesa Samwel Manyele akiwataka Watanzania kuacha kutumia mafuta ya
ubuyu kwa maelezo kuwa yana kemikali yenye madhara kwa afya ya binadamu.
Profesa Manyele alipinga kauli iliyotolewa na
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road mwanzoni mwa wiki hiyo wakati huo kwamba
mafuta hayo hayana madhara katika mwili wa binadamu yakitumiwa vizuri.
Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wakati huo, Dk Seif Rashid, alitangaza kuwa mafuta
hayo si salama na kusisitiza kuwa huo ndiyo msimamo wa serikali kuhusu mafuta
hayo, hivyo wananchi waamue wenyewe kuyatumia au kutokuyatumia.
Akizungumza
na BANDA BLOG, Profesa Manyele alisema,
“Ofisi
yangu inaiunga mkono kauli ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuzuia
matumizi ya mafuta hayo, Watanzania wanatakiwa kuwa wasikivu na onyo hilo.”
Alisema
sheria inayoruhusu mtu yoyote kufanya biashara ya chakula na dawa ipo chini ya
TFDA, wao ndio wanaotoa kibali cha kufanya biashara na kutengeneza bidhaa,
kwamba wakisema bidhaa fulani haifai wanatakiwa kusikilizwa.
“Wao
ndio wanaotoa kibali cha kutengeneza bidhaa, pia wana uwezo wa kuzuia uzalishaji
kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Mkemia Mkuu haiwezi kuzuia uzalishaji.”
Aliongeza
kuwa tayari TFDA imeshaeleza athari ya kemikali iliyopo katika mafuta ya ubuyu
inayoweza kuathiri afya za Watanzania, kuwataka wananchi kuwa makini na kama
wanahitaji taarifa za msingi wanatakiwa kwenda katika ofisi za mamlaka hiyo.
“Mimi
kama Mkemia Mkuu wa Serikali nitaingilia kati kama mambo yote yatashindikana na
serikali itataka kutoa tamko rasmi kuhusu matumizi ya mafuta haya.”
Binafsi
naona kuwa swali ambalo bado limebaki kwa kipindi cha miaka inayokaribia 10 kwa
sasa je kwanini Ocean Road kwa upande
wake na TFDA ya wakati huo kwa pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa nini kila
mmoja alipita njia yake katika hilo?
Kama
hoja ni madhara mbona sigara, tumbaku, pombe zina madhara kwa binadamu lakini
hazijapigwa marufuku bali tu imekwa sentensi katika bidhaa hizo kuwa zina
athari kwa afya ya mtumiaji?
Kwa
hakika hata kama kuna kemikali ndani ya mafuta hayo, kwa maendeleo ya sayansi
ya sasa inaweza kuondolewa kwa kutumia vifaa bora ili kuisaidia jamii kuendelea
kuyatumia mafuta hayo na hilo litasaidia kukuza hata uchumi wa maeneo ambayo
mibuyu inastawi kwa wingi.
Kwa
maana ya mazungumzo ya ndugu hawa, wao walikuwa wakitumia unga wa ubuyu na
mafuta yake kama kiungo kwa miaka mingi wamezaliwa wakiona mababu na mabibi wanautumia
unga na mafuta hayo iweje ulipigwa marufuku?
Mwanakwetu
ushauri wangu hasa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Ocean Road na TFDA mpya ya sasa
watoe wataalamu ambao ni wazaliwa wa asili ya mikoa ya Dodoma, Singida na hata
Iringa wakae pamoja walitazame jambo hilo alafu watoke kuielezea jamii ya
watumiaji wa kiungo hicho na hatua kadhaa
za maboresho ya kiungo hicho ili kuondoa utata kwani nimebaini kuwa kiungo
hicho bado kinatumika kwa siri.
Mwanakwetu
nalisema
hilo kwa kuwa itambulike waziwazi kunaga ubaga kuwa namna ya kupika na kula
vyakula ni sehemu ya utamaduni wa makabila yetu. Kupiga marufuku haitoshi, elimu
ya kina inahitajika zaidi isitoshe hata huko kupishana kwa wataalamu kunajenga
hoja nyengine.
Nakutakia
siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257