MNAONA MAMBO YENU !
Adeladius
Makwega-TANGA
Katika
siku kadhaa nimekuwa nikiona picha za vijana wanaokimbiza Mwenge wa Uhuru na
nimekuwa nikifuatilia maoni juu ya mwenge huo kila unapopita. Huku nikijiuliza Je
kweli Julius Nyerere na wenzake walipoanzisha dhana na Mwenge wa Uhuru nia yao
ilikuwa mwenge huu ulalamikiwe kama unavyofanyiwa sasa?
Je
huko ni kuwatendea haki ndugu hawa au wazo lao ililikuwa halina tija yoyote kwa
taifa letu?Je mzigo huo wa lawama ni wa vijana wanaoukimbiza mwenge huo, wizara
inayosimamia au CCM yenye serikali hiyo?
Lawama
dhidi ya Mwenge wa Uhuru mara zote nilichobaini zimekuwa ikitwikwa kichwani CCM
japokuwa makosa hayo huwa haifanyi yenyewe. Mara zote kwenye mwenge CCM huwa ni
mwalikwa tu.

Nakumbuka,
mwaka 2019 Mwenge wa Uhuru ulizinduliwa katika mkoa wa Songwe vizuri sana na
Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan. Baadaye vijana waliokuwa
wanaukimbiza walianza kazi hiyo katika wilaya ya Mbozi. Wilaya hiyo ilikuwa na
miradi zaidi ya mitano.
Katika
siku hiyo ya kwanza kati ya miradi hiyo miradi mitatu ilikataliwa likiwamo
Daraja Moja la TARURA, Darasa Moja la ELIMU SEKONDARI na Zahanati Moja ya AFYA.
Msomaji wangu naomba mradi wa barabara na darasa iwekwe kando nikusimulie
simulizi ya mradi mmoja tu uliokataliwa wa Zahanati ya Igunda,

Kijiji
cha Igunda kilikuwa hakina zahanati kwa miaka mingi huku wanakijiji wake wakipata
hisani ya kutibiwa katika vijiji vingine ndani ya kata ya Mlowo ambao ni mji
mkubwa wa Kibiashara katika mkoa mpya wa Songwe uliopo kandokando ya barabara
kubwa ya kwenda Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Wananchi
walihamasishwa na wakaitika vizuri na kuweza kujenga zahanati hadi kiwango cha
upauwaji, hapo serikali ya wilaya ikaongeza fedha za kumalizia hiyo zahanati
huku mfanyabiashara mmoja anayejulikana kama MARMO GRANITES akajitolea malumalu
nyingi kuukamilisha mradi huo kwa ubora zaidi.
Wakati
huo tayari madirisha ya aluminiamu yalikuwa yamepachikwa vizuri na jengo kuwa
limekamilika kwa kiwango cha juu kabisa. Binafsi sikuwahi kuona zahanati bora
kama hiyo kwa mjini na hata kijijini.
Serikali
ya wilaya ikapeleka watumishi, dawa na vifaa tiba ili Mwenge ukizindua huduma
ziendelee.Wananchi wa eneo hilo ambao wengi walikuwa wanaunga mkono siasa za
upinzani wakiongozwa na CHADEMA walishirikiana vizuri na CCM kukamilisha kazi
hiyo. Eneo hilo lilikuwa na diwani na CHADEMA na mbunge wa CHADEMA.
Wananchi
wa kata hii ambao wengi walikuwa Wanyia na Wanyakyusa wakiwa ndugu wa damu
waliondoa tofauti zao za kisiasa za uchaguzi wa mwaka 2015 na kuwa kitu kimoja
katika maendeleo.
Mara
baada ya Makamu wa Rais kuondoka tu Mwenge ukaondoka uwanjani hadi Igunda
wakimbiza mwenge walipofika hapo wakaukagua mradi, mwisho wa siku wakakataa
kufungua mradi huo.
“Siufungui
mradi huu, upo chini ya kiwango.”
Alisema
kiongozi wa wakimbiza mwenge.
Wananchi
waliguna mmmmmm! wakazima muziki ikawa kimya watu wakaanza kurudi majumbani
mwao.
Mimi
nilikuwa jirani na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbozi anaitwa Mzee Mboya. Huyu
ni mtumishi wa umma mstaafu. Kwa bahati nzuri Mzee Mboya anazaliwa kata ya Mlangali, hii ni kata yenye
Kimondo cha Mbozi, Mlowo na Mlangali ni kata jirani sana, hata kwa mguu unaenda
na hawa wote ni ndugu kabisa wa damu.
Nikiwa
jirani na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, akaja mtu mmoja jirani yetu kabisa
akamsalimia kwa Kinyia alafu akasema maneno haya,
“Si
mnaona CCM mambo yenu yalivyo? Mwenyekiti!, Yaani sisi kujituma kote kule leo
anakuja mtu anaukata mradi wetu?Eti Siufungui mradi huu, upo chini ya kiwango!
Kweli mradi huu utafanya kazi ? ”
Hata
mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbozi na yeye hakulidhishwa na mradi ule
kukataliwa lakini alitumia hekima kukaa kimya, mimi nikamjibu ndugu yule kuwa mradi
huu umeshaanza kufanya kazi leo hii na utaendelea kufanya kazi, kama kutakuwa
na maagizo mengine yatapokelewa. Binafsi pale nilijibu kwa niaba ya Serikali
nilikuwa mtu sahihi kulijibu swali hilo wakati huo.
Mwanakwetu
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya alibebeshwa mzigo mzito wa lawama kwa maamuzi ya
mkimbiza Mwenge.Yule aliyeuliza alikuwa ni kiongozi wa CHADEMA wa kata huku
alikuwa amevalia skafu ya chama hicho.
Mwenyekiti
Mboya akaniambia kuwa jambo hili limeshaleta tabu hapa itabidi nirudi baada ya
juma moja niongee na hawa ndugu zangu wote bila ya kujali vyama vyao.
Mzee
Mboya alifanya hivyo na kuwaeleza kuwa watu wa Igunda kuwa nia ya CCM ya kuwa
na Mwenge siyo kuleta mgawanyiko bali kuwa pamoja, aliomba ndugu zake na jambo
hilo likaisha na hadi sasa Zahanati ya Igunda inafanya kazi vizuri,
Mwanakwetu
Zahanati ya Igunda hata mtu akienda leo hii ni miongoni mwa zahanati bora za
umma nchini.Kilichofanyika ni kuondoa jiwe lenye jina la mkimbiza mwenge na
huduma kuendelea kama kawaida..
Swali
la kujiuliza je Mkimbiza Mwenge anajua hali aliyoiacha baada ya kuukataa mradi
huo na kazi kubwa iliyofanya na CCM baada ya tukio hilo?
Au
Kazi ya CCM ni kubebeshwa lawama kwa makosa yanayofanywa na watu wengine?
Binafsi
nilikwenda mbali zaidi, nilifuatilia hata alipotokea mkimbiza mwenge huyo, nilibaini
kuwa hata kwao alipotokea wanatumia zahanati moja ya zamani ambayo hata
ukarabati wake ulikuwa hafifu
Binafsi
ninaona kuwa dhana ya kuikata miradi kwa wakimbiza mwenge haina tija inabomoa
badala ya kujenga. Kwani hata kama mradi unakataliwa kwa faida ya nani?
Kama
kweli mradi huo upo chini ya kiwango Rais kila eneo anawawakilishi kadhaa katika kila
pahala watimize wajibu wao na mradi huo uondolewe kabla ya kiongozi wa mwenge
hajafika na kinyume chake CCM itabebeshwa mzigo ambao si wake kila wakati.
Mwanakwetu
japokuwa miradi hiyo mitatu ilikataliwa lakini wananchi wa wilaya hii jioni
yake walijitokeza kwa wingi kufurahi pamoja na wenzao huku Christian Bella-Best
of The Best akitumbuiza katika Viwanja vya Mlowo kwa nyimbo kama MSALIMITI, MAMA,
NAKUHITAJI, NASHINDWA, USILIE, YAPO WAPI MAPENZI na zingine nyingi usiku kucha.