SERIKALI NA WADAU WA NGOs WAJADILI NAMNA YA KUPUNGUZA UTEGEMEZI
Na WMJJWM Arusha
WADAU wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali
nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kutoa maoni katika Mkakati
wa Mashirika hayo ili kupunguza utegemezi katika utekelezaji wa miradi yao
Rai hiyo imetolewa jijini Arusha na Naibu
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi
Ali Khamis wakati akifungua kikao kazi cha wadau wa NGOs cha kujadili na kutoa
maoni katika Mkakati wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupunguza utegemezi kwa
wafadhili.
Mhe. Mwanaidi alisema mpaka sasa Kamati imekamilisha
andiko la majadiliano (Consultation Paper), nyenzo za ukusanyaji wa taarifa na
maoni kutoka kwa wadau mbalimbali (Stakeholders Engagement Tools), pamoja na
ukusanyaji wa taarifa na maoni kutoka kwa wadau na zoezi hilo linaendela katika
Kanda ya Kaskazini, Kanda ya nyada za Juu Kusini na Kanda ya Kati.
Mwanaidi aliwataka kuzingatia umuhimu wa Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali katika maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla, hivyo
alitoa rai kwa washiriki wa mkutano huo kutoa maoni yatakayosaidia kupatikana
kwa mkakati huo pia kushirikiana na kamati kwa hali na mali ili kuweza
kukamilisha mkakati utakaosaidia kukidhi malengo ya kuanzishwa kwa Mashirika yao
na matarajio ya jamii ya watanzania wanayohudumia.
Aidha Mhe. Mwanaidi alisema Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali ili kuwaletea Wananchi
wake maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi ya afua mbalimbali zikiwemo za Afya,
Kilimo, Elimu, Maji, Mazingira, Miundombinu, Utawala Bora, Nishati, hifadhi ya
Jamii, Mifugo na Uvuvi, Uwezeshaji wa Jamii na Sekta nyingine
mtambuka.
”Miradi hiyo, sio tu imewanufaisha Wananchi wetu kijamii,
bali pia imechangia katika kuongeza ukuaji wa uchumi, kuboresha utoaji wa
huduma na kuongeza fursa za ajira hususan kwa vijana, wanawake na watu wenye
ulemavu“alisema Naibu Waziri Mwanaidi
Akitoa taarifa ya Kikosi kazi cha kukusanya maoni juu ya
Mkakati wa NGOs kupunguza utegemezi, Katibu Mkuu wa Baraza la Mashirika Yasiyo
ya Kiserikali Revocatus Sono alisema Kikosi kazi hicho kimefanikiwa kuwafikia
wadau Zaidi ya 700 katika Knda ya Ziwa, Mashariki na Kaskazini hivyo
amewahimiza wadau hao kuendelea kushirikiana na Kikosi kazi hicho ili kuapata
maoni yatakayosaidia kupata Mkatati huo muhimu kwa ukuaji wa sekta ya NGOs.
Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa NGOs, Mkurugenzi
Msaidizi sehemu ya Usajili Mussa Sang’anya alisema Wizara inaendelea na
mchakato wa kukusanaya maoni kwa wada katika Kanda mbalimbali kwa kasi ili
kufikia malengo yake ya kuwasilisha rasimu ya Mkakati huo kwa Viongozi wa
Wizara kwa hatua zaidi za utekelezaji wake.
Kwa upande wake Msajili Msaidizi na Afisa Maendeleo ya
Jamii mkoa wa Arusha Blandina Nkini ameishukuru Wizara kwa kuratibu zoezi hilo
ambalo muhimu katika maendeleo ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchuni kwanin
itayasaidia kupunguza utegemezi na kuwa na muendelezo wa utoaji wa huduma na
utekelezaji wa miradi na majukumu yao.
“Nitoe pongezi kwenu Wizara katika hili hakika mmefanya jambo litakalokumbukwa na vizazi kwa kuweka namna bora itakayosaidia kuokoa NGOs ambazo ufadhili ukipungua au kumalizika zinakosa muelekeo na nyingine zinakufa na kuacha wananchi wakihitaji huduma za NGOs hizo” alisema Blandina
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi
Maalum inashirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali
(NaCoNGO) kuratibu zoezi la utaoji maoni ya wadau wa NGOs katika kuwa na
Mkakati wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupunguza utegemezi na linaendeshwa
katika kanda tano za Mashariki, Kati, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Ziwa.
MWISHO
|
|
|