Mwenyekiti wa Baraza la Taifa akizungumza kwa niaba ya Viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka Mikoa ya Tanzania Bara katika Mkutano kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula na Wawakilishi wa viongozi wa mabaraza hayo katika Mkutano uliofanyika Mei 17, 2022 jijini Dodoma.
Baadhi ya Wawakilishi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara katika Mkutano kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula na Wawakilishi wa viongozi wa mabaraza hayo katika Mkutano uliofanyika Mei 17, 2022 jijini Dodoma.Na WMJJWM - Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt Zainab Chaula amesema kuwa Wizara
imepanga kuanzisha Makazi ya Wazee kikanda ili kuweka mazingira mazuri ya
kuwalea Wazee wasiojiweza nchini.
Dkt. Chaula ameyasema hayo Mei 17, 2022 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara.
Dkt. Chaula alisema kuwa Wizara
imejipanga kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya kuwalea Wazee wasiojiweza na
Ustawi wa Wazee kwa ujumla.
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha
2022/23 Wizara imejipanga kuanza kukarabati baadhi ya Makazi ya Wazee ili
kuwezesha kuwa na Makazi hayo katika Kanda, hali itakayosaidia kuwa na Uratibu
na huduma Bora zaidi kwa Wazee wasiojiweza chini.
"Hili ni muhimu sana na Wizara ipo
katika mikakati ya kuboresha utoaji huduma katika Makazi ya Wazee
inayoyaendesha kwa kuyaratibu kikanda ili kuwe na ufanisi na ubora katika
huduma" alisema Dkt. Chaula
Akizungumza baada ya
ufunguzi wa Mkutano huo Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii anayeshughulikia
masuala ya Wazee Tullo Masanja, alisema lengo la kuwakutanisha Wawakilishi wa
viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara, ni kuwa mabalozi
kwa wenzao katika kutoa maoni kuhusu Sera ya Wazee ili iwe jumuishi katika
utoaji maoni kwa lengo la kuwa na Sera iliyo Bora.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la
Taifa la Wazee David Lameck Sendo alisema Viongozi wa mabaraza ya Wazee
Tanzania Bara wameamua kukutana ili kuweka mikakati mbalimbali inayolenga
kuboresha Usatwi wa Wazee ikiwemo kupitia rasimu ya maboresho ya Sera ya Wazee
nchini na kutoa maoni yao katika Sera hiyo.
"Lingine la muhimu ni kuwa
na Muongozo wa uendeshaji wa Mabaraza ya Wazee nchini kwani itasaidia kuwa na
uelekeo sahihi na wenye tija katika kuendesha mabaraza hayo" alisema David
Lameck Sendo
Kwa upande wake Mwakilishi wa
Shirika la Help Age Joseph Mbasha alisema Shirika hilo linashirikiana na
Mitandao ya Wazee na Serikali katika kuhakikisha wanatoa rasilimali mbalimbali
ili kusaidia jitihada za Serikali za kuwawezesha Wazee kupata huduma Bora katika
Sekta mbalimbali ikiwemo Afya na kuwezesha Wazee hao kukutana kuzungumza na
kujadiliana changamoto zao kupitia mabaraza ya Wazee.
Nao baadhi ya Wazee walisema
Mkutano huo umekuja kwa wakati sahihi ambapo Wazee walio wengi amekuwa na
matamanio ya kuwa na Sera itakayosaidia kuleta Ustawi wa Wazee nchini ikiwemo
namna bora ya kuwatunza na kuwaenzi Wazee.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii
imewakutanisha Viongozi wa mabaraza ya Wazee kutoka mikoa ya Tanzania Bara kwa
lengo la kuwapitisha katika masuala mbalimbali yahusiyo Ustawi wa Wazee nchini.
MWISHO