UMILIKISHAJI ARDHI KUONDOA CHANGAMOTO KWA WANAWAKE-NAIBU WAZIRI
RIDHIWANI
Na Anthony Ishengoma na Munir Shemweta, WANMM MBEYA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Ridhiwani Kikwete amesema faida kubwa na kipaumbele katika zoezi la
Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi ni kupambana na ukatili dhidi ya wanawake
ikiwemo kuondoa changamoto ya akina mama kukosa nguvu ya kumiliki ardhi haki
aliyoieleza kuwa itapatikana kwa kutoa hati ya pamoja kati ya mume na
mke.
Naibu Waziri Kikwete amesema hayo Mei 13, 2022 wakati akihutubia
wananchi wa Mbalizi Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wakati wa uzinduzi wa mradi
wa Kupanga, Kupima na Kumilikishwa ardhi unaosimamiwa na Chuo cha Ardhi
Morogoro (ARIMO) na baadae kushiriki zoezi la ugawaji hati kwa wananchi
waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.
Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa, Kupima ardhi kutawezesha kutatua
migogoro isiyo ya razima kwa kuwa kazi hiyo inahusisha upimaji shirikishi ambao
baada ya wataalamu kujiridhisha wakati wa zoezi hilo hati hutolewa bila ya
kuwepo migogoro yoyote.
‘’Kumekuwepo na spidi ndogo ya wananchi kwenda kuchukua hati zao
lakini niwambie ninyi kuna wakati utafika mutahitaji kulima kadiri ya taratibu
za serikali na kuepuka uharibifu wa mazingira kuna wakati itabidi zitumike
mbinu za kitaalam ili kuendelea na kilimo.’’Aliongeza Ridhiwani
Kikwete Naibu Waziri Wizara ya Ardhi.
Naibu Waziri Ridhiwani alizitaja faida za kuwa na hati kuwa ni
pamoja na kuthaminiwa na kupatiwa uhakika wa kupata huduma za kibenki kwa
mmiliki, kuongeza thamani ya ardhi tofauti na ile ardhi isiyopimwa aliyoieleza
kuwa haina thamani yoyote hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Bw. Huruma
Lugalla amesema chuo chake kilikopeshwa kiasi cha Tsh. Bil 1.2 kwa ajili ya
program ya Kupima, Kupanga na Kumilikisha Ardhi kwa wakazi wa Mbalizi mkoani
Mbeya ambapo viwanja takribani 35,000 tayari vimepimwa.
Kwa mujibu wa Lugala, kiasi hicho cha fedha walizopatiwa tayari
kimewezesha upimaji na utambuzi wa viwanja 31,06 sawa na 89% katika lengo
lililokusudiwa.
Aidha Mkuu huyo wa Chuo cha Ardhi Morogoro, aliongeza kuwa
upimaji wa viwanja hivyo ulienda sawia na uandaaji wa michoro ya mipango miji
na tayari michoro 108 kati ya 120 ambayo ni sawa na asilimia 90% imesanifiwa na
kati ya hiyo michoro 80 imewasilishwa ofisi ya Kamishna wa Ardhi wa Mkoa kwa
ajili ya idhini.