WUSM
MILANGO IPO WAZI–KAIMU KATIBU MKUU JANABI

Adeladius Makwega-WUSM
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini ndugu Haji Janabi amesema kuwa milango ya wizara
hii ipo wazi kwa kila Mtanzania kufika kuzifahamu kwa kina sekta zinazosimamiwa
na wizara hiyo.
Ndugu Janabi ameyasema hayo
Mei 18, 2022 Mtumba-Mji wa Serikali Jijini Dodoma wakati akizungumza na
wakaguzi wa nje kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
wakiwa pamoja na wakuu wa idara na vitengo wa wizara hiyo katika kikao maalumu
cha ukaguzi wa mali za zamani za serikali.
“Wizara yetu tunajishughulisha
kwa kina na Utamaduni wetu, Sanaa yetu na Michezo yetu na ndiyo maana hapa ninao
wakurugenzi wote wa sekta zetu, wapo pamoja na wakuu wa vitengo ili watoe ushirikiano kwa kila litakalo hitajika
na kuulizwa tangu mwaka 2011 hadi sasa kwa mali hizo za zamani.”
Aliongeza kwa kuwa zoezi hilo
limepitia hatua mbalimbali ana hakika linafanyika na litakamilika kwa ufanisi
mkubwa.
“Ukiona ngoma makao makuu
hapa, ukiona muziki makao makuu hapa hapa na hata ukiona michezo makao makuu
hapa, karibuni pia kujifunza haya mambo yetu njia ni nyeupe na mlango
umefunguliwa kwenu na kwa kila Mtanzania.”
Kaimu
Katibu Mkuu Janabi ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sera na Mipango wizarani hapa aliongeza kuwa wizara hii katika kutekeleza majukumu
yake kikamilifu kimuundo imegawanyika katika maeneo makuu mawili moja ni
usimamizi na utekelezaji wa masuala ya kisekta na pili ni uendeshaji, uratibu
na usimamizi.
Kikao hicho kilikamilika kikamilifu na kutoa wasaa kwa wakaguzi
hao kufanya kazi yao na wakuu wa idara na vitengo wizarani hapa kutoa
ushirikiano na kujibu litakalo ulizwa.