Felix-Antoine Tshisekedi Tshilombo, rais wa DRC, ni nani?
Felix Tshisekedi anagombea uchaguzi wa urais wa DRC akiongoza muungano wa ''Union Sacree'' wenye vyama zaidi ya 500 katika nchi nzima./ Picha: AFP
Felix Tshisekedi ni rais wa kwanza kuchukua hatamu ya
uongozi kupitia njia ya kidemokrasia tangu Jamhuri hiyo ya Kidemokrasia ya
Kongo kujinyakulia uhuru 1960.
Tshisekedi, aliye na miaka 60, ni mtoto wa kati katika
familia ya watoto watano, ni mrithi wa kisiasa wa marehemu baba yake Étienne
Tshisekedi, aliyekuwa mwanasiasa mkongwe nchini DRC.
ÉtienneTshisekedi wa Mulumba alianzisha chama cha 'Union
Pour la Démocratie et le Progrès Social' (UDPS), mnamo1982, kilichokuwa chama
cha Upinzani kupinga utawala wa Mubutu Sese Seko aliyekuwa madarakani wakati
huo.
Harakati za kisiasa za Tshisekedi 'mkubwa' zilimpelekea
kuwekwa korokoroni mara nyingi na hivyo basi familia kulazimika kuhama Kinshasa
na kwenda kujificha katika kijiji chao cha asili katika eneo la Kassai.
Hata hivyo, hiyo haikuwa dawa kwani masaibu yaliendelea
kuwaandama.
Mnamo 2011, Étienne Tshisekedi alichaguliwa kuwa mbunge
wa jimbo la Mbuji-Mayi katika eneo la Kassai. Mwaka huo, Baba yake Étienne
alishindwa uchaguzi na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Joseph Kabila.
Mzee Étienne Tshisekedi alifariki dunia tarehe 1 Februari
2017 nchini Ubelgiji na kuzikwa miaka 2 baadaye.
Baada ya kifo cha baba yake mnamo 2017, Tshisekedi mtoto
alirithi chama kilichoongozwa na babake cha 'Union pour la Démocratie et le
Progrès Social' UDPS.
Alilikumbatia jukumu hilo kikamilifu na hata kujijengea
safari ya kisiasa na kuwa mgombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi wa
urais wenye utata mnamo 2018.
Kufuatia makubaliano ya mwaka 2017 kati ya serikali na
upinzani maarufu ''Accords de Saint Sylvestre,'' jina lake
lilitajwa kuwa na uwezekano wa kushililia wadhifa wa waziri mkuu, lakini
hatimae rais wa kipindi hicho Joseph Kabila alimchagua Bruno Tshibala.
Hata hivyo, Felix Tshisekedi hakuvunjika moyo kwani
aliendeleza na harakati zake za kisiasa na kuchukua uongozi kamili wa chama cha
UDPS na hata kuwa mgombea wa Chama kwenye kinyanganyiro cha uchaguzi mkuu wa
2018.
Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi wa urais kwa kupata
asilimia 36 ya kura na kutawazwa mshindi mnamo tarehe10 Januari 2019 kuwa rais
wa tano wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Tshisekedi alihudumu muhula wa kwanza ingawa kipindi
chenyewe kilikumbwa na migogoro ya kivita na kisiasa hasa eneo lake la
mashariki.
Mnamo 2021, Tshisekedi alichaguliwa mwenyekiti wa AU
katika kikao cha kawaida cha 34 kilichofanyika kati ya tarehe 6-7 Februari na
kuchukua nafasi ya rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.
Felix Tshisekedi alipata elimu ya msingi na sekondari
mjini Kinshasa licha ya kukatizwa shule akiwa na umri wa miaka19 kutokana na
misukosuko ya kisiasa iliyomsibu babake.
Akiwa na umri wa miaka 22, Felix Tshisekedi pamoja na
mama yake na ndugu zake, walipata hifadhi mjini Brussels, nchini Ubelgiji na
hapo ndipo alipopachikwa jina lake la Utani la ''Fatshi'' ambalo anafahamika
nalo hadi leo.
Tshisekedi 'akajiunga' na Chuo Kikuu na kusoma katika
Kitivo cha Masoko na Mawasiliano.
Mkewe rais Tshisekedi ni Denise Nyakuru kutoka mji wa
Bukavu, Kivu Kusini, ambaye wamejaliwa watoto watano kwenye ndoa yao ya miaka
23. Wanne wa kike ambao ni Fanny, Christina, Sabrina na Serena. Antony ndio
mtoto pekee wa kiume wa rais Tshisekedi.
Tsishekedi ameingia uchaguzi uliomalizika wa DRC wa
Disemba 20 na kauli mbiu ya kurudisha hadhi na uhuru wa DRC ikiwemo kupambana
na makundi yote ya waasi kama vile M23.
