KRISIMASI INATUKUMBUSHA KUTIMIZA
WAJIBU-PADRI MASANJA
Adeladius
Makwega-MWANZA
Wakristo wameambiwa kuwa kuzaliwa Kwa Yesu Kristo
kulikuwa na dhumuni la kuleta amani zaidi kwa mwanadamu ambalo ni tukio
lililotokea miaka zaidi ya 2000 iliyopita , hivyo kwa sherehe ya Noeli kila
mwanadamu anatakiwa kuwa na furaha zaidi na kujipanga upya huku kila mmoja
kutimiza wajibu wake, maana mkombozi amezaliwa.
Hayo yamesemwa katika misa ya mkesha wa Noeli
katika Mlima wa Hija, Disemba 24, 2023 kuamkia Disemba 25, 2023 kando ya viunga
vya Parokia ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Padri Samsoni Masanja ambaye
ni Paroko wa Parokia hiyo .
“Furaha inayotakiwa na kupokelewa ni ya kuzaliwa
Yesu Kristo na iwe katika mioyo yetu na furaha hiyo idhilike katika kila yeye
anayesherekea sikukuu hii.”
Akiendelea kuhubiri katika misa hiyo Padri Masanja
alisema kuwa Familia ya Yusufu, Maria na Yesu ni Familia Bora na siyo Bora Familia
na ndiyo maana hii ni Familia Takatifu.
Usiku wa mkesha huu wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo
kila mmoja anawajibu wa kuiga mfano huo na kuwa na Familia Bora inayotimiza
wajibu wa kila mwanafamilia.
“Katika injili ya leo tunaambiwa Yesu Kristo alipozaliwa
tu alivishwa mavazi ya kitoto, maana yake wazazi wake walitimiza wajibu wao ipasavyo.
Eee na wewe muumini unatimiza wajibu wako kwa familia yako ? Iwe katika mavazi,
maladhi na chakula? Unakutana na mtoto amevaa vilaka huku tochi zinamulika,
hilo halikubaliki na siyo mafundisho ya Ukristo, wakati baba/mama/ mlezi anavaa
vizuri, huku watoto wakiwa na hali mbaya, jamani imani yetu inatufundisha
kutimiza wajibu wetu ipasavyo, iwe kwa baba, mama na hata watoto.”
Akihubiri usiku huo, Padri huyu kijana aliweza
kutoa mahubiri yaliyowaingia vizuri waamini wake, huku akichanganya Kiswahili
na Kisukuma ambapo kwa hakika kila alipouliza swali iwe kwa Kiswahili au
Kisukuma nao waamini walijibu kwa lugha iliyoulizwa.
Padri Masanja alisema kuwa mwaka mpya wa 2024
umekaribia, hivyo kama kuna mlei hajajipanga vizuri kwa mwaka kwa mwaka mpya
ajipange sasa na kama hakufanya vizuri kiroho na kimwili kwa mwaka 2023
ajipange vizuri maana Sikukuu ya Noeli inatukumbusha kutimiza wajibu wetu maana
Bwana Wetu Yesu Kristo amezaliwa.
Misa hiyo iliyoanza saa nne kamili ya usiku
ilikamilika majira ya saa 9 usiku, huku watoto kadhaa wakibatizwa na ikuhudhuliwa
na viongozi kadhaa wa Hija wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Makatekista na
walei, nayo historia ya kuingia Ukristo Tanzania ikisomwa, ambapo Mlima wa Hija
hapa Malya Wamisionari wa kwanza walisali Krisimasi ya kwanza wakati Ukristo
Ukatoliki ulipokuwa unaingia Jimbo Katoliki la Mwanza mwaka 1878.