Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Umoja wa Afrika unaunda mfumo wa kusaidia nchi ambazo
zimesimamishwa kwa muda katika Umoja wa Afrika ili ziwe katika kipindi cha
mpito wakati zikijiandaa kufikia utawala wa kidemokrasia.
Baraza la Amani na Usalama la AU, lenye wajumbe 15,
lilifanya mkutano wake katika mkutano wa kila mwaka wa marais, nchini Ethiopia
tarehe 17 na 18 Februari 2024.
"Tutafanya kazi na wahusika wengi ikiwa ni
pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNDP, katika uzinduzi wa kile
tunachokiita "Mfumo wa Afrika," hii ni kusaidia mabadiliko ya amani
barani Afrika," anasema Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika,
Bankole Adeoye.
Hadi sasa nchi sita za Afrika zilizo uanachama wao
umesimamishwa kwa muda Umoja wa Afrika ni Gabon, Niger, Guinea, Sudan, Burkina
Faso, na Mali. Wote wako chini ya utawala wa kijeshi.
Sheria ya AU inaunga mkono utawala wa kiraia katika
nchi wanachama wake.
"Hatua hii inakuza ushirikiano wa jinsi nchi
wanachama waliosimamishwa kwa muda kutoka AU, wanaweza kuwa na mpito wa kisiasa
bila changamoto. Kwa hivyo, tunafanya kazi na nchi husika katika suala la
ajenda yao ya mpito wa kisiasa ili waweze kurejea AU. Hii ni kwa masharti
kwamba waheshimu utaratibu wa kikatiba na kufanya uchaguzi huru, haki na
uwazi,” Adeoye anaongeza.
Vikwazo hutolewa kufuatia sheria zinazosimamia
muungano wa bara. Walakini, wataalam wanatilia shaka ufanisi wao.
"Lakini nyakati zimebadilika, na viongozi wa
kijeshi wana sababu kidogo sana ya kuogopa kutokuwa katika Umoja wa
Afrika," hayo ni kwa mujibu wa uchambuzi wa Crisis Group. International
Crisis Group ni Shirika Huru linalofanya kazi kuzuia vita na kuunda sera ambazo
zitajenga dunia yenye amani zaidi.
"… Ulimwengu wa ushindani mkubwa wa kijiografia
unafanya iwe rahisi kwao kuhusiana na nchi tofauti za kigeni kwa manufaa yao ya
kisiasa," imeongeza.
Nchi za Afrika Magharibi - Mali, Niger na Burkina
Faso zimefanya uamuzi wao wa kujiondoa mara moja kutoka kwa Umoja wa Afrika
Magharibi, ECOWAS, ambacho ni chombo cha utekelezaji cha AU.
Wamelalamikia masuala tofauti ikiwemo kile
wanachokiita kutotendewa haki na ECOWAS.
Lakini Umoja wa Afrika unaonekana bado una nia ya
kuweka vikwazo kama kipaumbele katika kushughulikia mabadiliko ya serikali
kinyume na katiba.
"AU haifanyi chochote kipya," anasisitiza
Adeoye," ni muhimu kutambua kwamba, ndiyo, wahusika wa mapinduzi ya
kijeshi wanaweza kutoa sababu mbalimbali kwa sisi katika AU kukiuka maadili
katika mifumo ya kawaida, lakini vikwazo vitaendelea kuwekwa kwa masharti ya
kusimamishwa kutoka AU."
Jopo la ngazi ya juu kwa Sudan
Mzozo wa Sudan ulifanikisha suala lililojadiliwa na
Baraza la Amani na Usalama la AU katika ngazi ya urais huku ikitajwa kama
"kipaumbele kikuu cha AU mnamo 2024".
Mapigano kati ya majeshi ya Sudan na Vikosi vya
Msaada wa Haraka tangu Aprili 2023 yameitumbukiza nchi hiyo katika kile ambacho
Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa "mgogoro wa dharura."
"Miezi kumi tangu mzozo huo kuibuka, nusu ya
wakazi wa Sudan - baadhi ya watu milioni 25 - wanahitaji msaada wa kibinadamu
na ulinzi. Zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbia mipaka ya Sudan hadi Jamhuri ya
Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini," hayo ni kulingana
na Shirila la Umoja wa Mataifa la UNHCR.
Juhudi za upatanishi zimegonga mwamba huku nchi hiyo
ya pembe ya Afrika, iliyosimamishwa uanachama wa Umoja wa Afrika, ikiamua
Januari 2024, kusimamisha uanachama wake kutoka kwa Mamlaka ya Kiserikali ya
Maendeleo IGAD.
IGAD ilipewa jukumu na Umoja wa Afrika kuongoza
juhudi za upatanishi kati ya pande zinazozozana.
Mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika 2024 umeidhinisha
kikundi cha ngazi ya juu kwa Sudan.
Kikundi hicho kitajumuisha Dkt. Mohamed Ibn Chambas,
Mwakilishi Mkuu wa AU anayehusika na mfumo wa AU wa " kunyamazisha
Bunduki, pia ni pamoja na Dkt. Specioza Wandira-Kazibwe, Makamu wa Rais wa
zamani wa Jamhuri ya Uganda na Balozi Fransisco Madeira, aliyekuwa Mwakilishi
Maalum wa Mwenyekiti wa Umoja huo nchini Somalia na aliyekuwa Mkuu wa ATMIS.
"Tuna watu katika kanda ambao wanaijua Sudan
hivyo wanaweza kuchangia kupata suluhisho. Ninaweza kuwahakikishia kuwa jopo
hilo sasa liko tayari kutekeleza shughuli zake kutoka kwa mkutano huu wa kilele
ili kuhakikisha kuwa washikadau wote ... nchini Sudan wanachangia katika
mazungumzo ya amani ya kisiasa,” Adeoye ameongezea.
Ni matumaini ya viongozi hao wa AU kuwa mazungumzo ya
kisiasa nchini Sudan yatasaidia kuhamasisha kuwaleta wadau wote mezani na
hatimaye kusitisha vita, nchini Sudan.
Umoja wa Afrika unatumai kuwa mwaka huu utasaidia
kuunga mkono nchi ambazo ziko chini ya utawala wa kijeshi kuweka utaratibu wa
wazi utakaosaidia kufanyika kwa uchaguzi ili mamlaka ziweze kuhamishiwa kwa ŕaia
na waweze kuŕejeshwa
tena kushiriki katika shughuli za Umoja wa Afŕika. 

