Mamlaka ya usafiri wa anga nchini Kenya
KCAA imethibitisha katika taarifa kwenye mtandao wa X kuwa ndege aina ya Dash 8
kutoka kampuni ya Safarilink imegongana angani na ndege ndogo ya wanafunzi aina
ya Cessna 172 mwendo wa saa tatu na robo asubuhi.
Hakuna maelezo kamili juu ya majeruhi au
vifo vyovyote kutoka kwa vyombo husika.
Ndege ya Safarilink ilikuwa safarini
kuelekea Diani, pwani ya Kenya ikiwa na abiria 39 na wahudumu watano huku ndege
ya mafunzo ya Cessna 172 inamilikiwa na chuo cha mafunzo ya urubani ya
Ninety-Nines.
Mamlaka ya KCAA imesema kuwa uchunguzi
umeanzishwa unaohusisha vyombo mbali mbali husika, ukiongozwa na idara ya ajali
za ndege nchini Kenya AAID, kujua chanzo cha ajali hiyo.
Awali kampuni ya Safarilink ilichapisha
taarifa katika mtandao wake wa X, zamani Twitter kuwa ndege yao moja
imelazimika kutua ghafla baada ya mlio mkubwa kusikika, japo hawakutaja iwapo
ilikuwa kugongana au mlipuko mwingine.
Walioshuhudia wanasema ndege hiyo ya
mafunzo ilianguka katika hifadhi ya wanyama ya Nairobi, iliyo karibu na uwanja
wa ndege wa Wilson.
