Rais Donald Trump wa Marekani aitaka NATO na washirika wengine kusaidia juhudi za kufungua Mlango Bahari wa Hormuz
Rais Trump aidha amesema huenda akauahirisha mkutano uliopangwa na Rais wa China Xi Jinping, akimshinikiza pia kusaidia mkakati huo.
Tahadhari hiyo ya Trump ilichapishwa kwenye gazeti la Financial Times jana Jumapili. Alinukuliwa akisema anadhani China pia inapaswa kusaidia kwa sababu inapata asilimia 90 ya mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz na kuongeza kuwa angependelea kujua nafasi ya Beijing kabla ya kwenda nchini China.
Waziri wa fedha wa Marekani Scott Bessent na Naibu Waziri Mkuu wa china He Lifeng jana Jumapili walikamilisha raundi ya kwanza ya mazungumzo yaliyofanyika kwa siku mbili mjini Paris, wakiangazia vizingiti katika utekelezaji wa makubaliano ya kibiashara pamoja na kuandaa mazingira ya ziara hiyo ya Trump anakotarajiwa kukutana na Xi mwishoni mwa mwezi Machi.
Amesisitiza kwamba mataifa yote yanayonufaika na ujia huo wanalazimika kuhakikisha unakuwa usalama.
Starmer na Trump wazungumzia hali Mashariki ya Kati, Hormuz
Awali, rais Trump alizungumza kwa simu na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer kuhusiana na umuhimu wa kuufungua tena Mlango huo. Ofisi ya Starmer imesema viongozi hao pamoja na suala hilo walijadiliana kuhusu hali ilivyo Mashariki ya Kati ili kukabiliana na kadhia ya usafirishaji na inayochochea kupanda kwa gharama kote ulimwenguni
