BANDA MEDIA BLOG

KASISI LUGENDO - THEOLOJIA YA KAZI KUCHOCHEA MAENDELEO YA JAMII NA KANISA


Na Rev. Maiko Luoga  – Morogoro

Washiriki wa Mkutano wa kwanza wa Kitaifa wa Theolojia ya Kazi ulioandaliwa na Chuo cha Biblia Morogoro (Morogoro Bible College) Dayosisi ya Morogoro, Kanisa Anglikana Tanzania, wametakiwa kufanyia kazi Elimu waliyoipata ili  kuchochea maendeleo.

Wito huo umetolewa hivi karibuni  na Kasisi Lugendo Msegu, Katibu wa Dayosisi ya Morogoro, wakati akifunga mkutano huo uliofanyika  katika Ukumbi wa CCT Kilakala mkoani Morogoro.

"Elimu Tuliyopewa hapa Tukaifanyie kazi kwa vitendo badala ya kukaa na ujumbe huu katika mawazo, Tutakuwa tumepoteza muda wa kuwepo hapa, Twende tukaitumie kuimarisha maendeleo ya Kanisa, Jamii na Taifa letu" alisema Kasisi Lugendo Msegu.

Mkuu wa Chuo cha Biblia Morogoro na mwanzilishi wa Theolojia ya Kazi nchini Kasisi Canon Dkt. Samwel Maduma alisema, Lengo kubwa la Mkutano huo ni kuandaa watumishi wenye kufundisha Kanisa Habari njema za Kristo pamoja na kuimarisha uchumi wa watu.

“Jamii imezungukwa na wingi wa watu wenye mafundisho potofu ya Neno la Mungu, Hivyo Tumekuja na wazo hili la Theolojia ya Kazi ili kusaidia watumishi wa Mungu kufundisha Neno lenye maarifa pamoja na kufundisha wakristo kufanya kazi kwa Bidii ili kuimarisha uchumi Binafsi, Kanisa na Jamii” alisema Kasisi Canon. Dkt. Maduma.

Akizungumza kwa niaba ya Wakufunzi katika Mkutano huo Kasisi Canon. Balozi Profesa. Emmanuel Mbennah alisema, Theolojia ya Kazi imekuja katika muda muafaka wa kulisaidia Kanisa kusonga mbele kiuchumi ili kuondokana na tabia Tegemezi hasa katika shughuli zinazotegemea fedha kutoka kwa waumini.

“Theolojia ya Kazi itusaidie Kanisa na Jamii kuona Fulsa za uchumi zilizopo katika maeneo yetu na kuzitumia kwa faida, Muumini akitoka Kanisani siku ya Jumapili, Jumatatu hadi Jumamosi afanye kazi za uzalishaji uchumi” alisema Prof. Mbennah.

Bw. Johnson Mgimba na Bi. Fidea Njama, Washiriki wa Mkutano huo walisema, Mada ya Theolojia ya kazi inapaswa kuungwa mkono na Wakristo watanzania ili kuitumia katika mazingira yao ya kazi na Makanisa ili kumtukuza Mungu kwa furaha siku zote.

“Hoja hii imekuja katika wakati ambao Watanzania tunapaswa kuipokea na kuunga mkono ili ipate nguvu katika Kanisa na Jamii, kwakuwa inatoa nafasi ya kumtumikia Mungu na kutumia fursa zetu kujiimarisha kiuchumi, Kimwili na Kiroho” Walisema.

Evelina Yotham na Christopher Kilumbo, Wanafunzi wa Chuo cha Biblia Morogoro walisema, Theolojia ya Kazi inawapa nafasi wanafunzi wa vyuo vya Biblia na vile vya Elimu za Kijamii nchini kujiandaa kikamilifu kuhudumia Jamii katika Nyanja tofauti.

“Tungependa Theolojia ya kazi iwe Somo rasmi la kufundishwa katika Vyuo mbalimbali nchini ili iweze kutusaidia sisi tunaojiandaa Kwenda kutumika katika Makanis ana Taasisi mbalimbali za Kijamii, Tunampongeza sana mwanzilishi wa Jambo hili Kasisi Can. Dkt. Samwel Maduma” walisema Wanafunzi hao. 




Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Mkutano huo Mhandisi Peter Chisawilo alisema pamoja na mambo mbalimbali ya maendeleo yaliyojadiliwa, Mkutano huo umetoka na maamuzi ya Kuunda Baraza la Kitaifa la Theolojia ya Kazi pamoja na kukubaliana kuwa kazi ni wito na jambo la kumrudishia Mungu Utukufu.

Mkutano huo ulifunguliwa Tarehe 20 Agosti 2026 na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Adamu Malima ambae aliwapongza na kuwataka washiriki kutoka Madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini kutumia mafunzo waliyoyapata kuimarisha uchumi wao, Kanisa na Jamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG