BANDA MEDIA BLOG

WATUHUMIWA WA MAUAJI NA WIZI WA PIKIPIKI WAFARIKI DUNIA WAKIPATIWA MATIBABU

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema huko maeneo ya Kijenge Jijini Arusha, limefanikiwa kupambana na kuwadhibiti watuhumiwa wawili waliokuwa wanatafutwa kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya kihalifu ikiwemo mauaji na uporaji hususani wa pikipiki.

Akitoa taarifa hiyo Oktoba 22, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 21, 2026 saa 03:30 usiku ambapo watuhumiwa hao walifariki dunia wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini kutokana na majeraha waliyoyapata wakati wa mapambano

SACP Masejo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Yusuph Hamis kwa jina maarufu Yuzo na mwingine ni Dickson Livingstone jina maarufu Ndesaa, ambao walijeruhiwa na Askari wakati walipokuwa wanajihami kwa silaha kuzuia kukamatwa, katika eneo ambalo walikuwa wamepanga kutekeleza tukio lingine la uhalifu.

Ameendelea kufafanua kuwa watuhumiwa hao walikutwa na silaha walizokuwa wanazitumia kwa ajili ya kujihami wasikamatwe ikiwemo bastola na panga, lakini pia walikutwa na pikipiki moja mpya isiyokuwa na namba za usajili kitendo ambacho ni kuficha kutambuliwa kwa urahisi.

Kamanda Masejo amebainisha kuwa mtuhumiwa, Yusuph Hamis @ Yuzo alikuwa anatuhumiwa kuongoza genge la uhalifu ambalo limekuwa likijihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo tukio la Mauaji ya Erasto Losujaki dereva bodaboda Mkazi wa Kisongo ambaye alikutwa amefariki dunia pembeni ya barabara tarehe 28.04.2026 katika kitongoji cha Olkaria, Kata ya Matevez Wilaya ya Arumeru huku pikipiki yake ikiwa imeporwa. 

Amataja tukio lingine ni la Mauaji ya Adiel Thomas Spitari, Dereva Bodaboda na Mkazi wa Ngaramtoni ambaye aliporwa pikipiki kisha kuuawa tarehe 15.09.2026 katika kijiji cha Likamba, Kata ya Musa wilaya ya Arumeru.

Pia, amesema watuhumiwa hao waliwahi kufikishwa mahakamani, kufungwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuvunja nyumba na kuiba na walitumikia vifungo mbalimbali ambapo mtuhumiwa Dickson livingstone @ Ndesaa alikuwa bado anaendelea kutumikia kifungo cha nje.

Jeshi hilo limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hio ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia watuhumiwa wengine waliokuwa wanashirikiana nao na kufuatilia mali zingine walizopora zikiwepo pikipiki.

Post a Comment

Previous Post Next Post
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG
BANDA MEDIA BLOG