Na. Lilian Lundo – Maelezo
17/3/2016. DAR ES SALAAM.
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika
ufunguzi wa Mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2016 yatakayofanyika
Machi 19, 2016 jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mashindano hayo
leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Lino International Agency Limited
kampuni inayoandaa mashindano hayo Bw. Hashim Lundenga amesema kuwa
uzinduzi huo kwa mwaka 2016 utakuwa wa aina yake tofauti na miaka
iliyopita.
“Tunatarajia kutangaza kamati
mpya ya Miss Tanzania siku hiyo ya uzinduzi, kamati ya Miss Tanzania
itakuwa na jukumu la kuusaidia uongozi wa Miss Tanzania katika shughuli
nzima za kuratibu na kusimamia mashindano hayo.” alisema Lundenga.
Lundenga ameongeza kuwa, katika
uzinduzi huo wadau mbalimbali wa tasnia ya urembo wakiwemo wabunifu wa
mavazi, mawakala wanaoandaa mashindano ya Miss Tanzania katika ngazi
mbalimbali hapa nchini watakutana .
Aidha amesema uzinduzi wa Miss
Tanzania mwaka 2016 umedhaminiwa na makampuni ya Ramada Resorts Dar,
Naf Beach Hotel Mtwara, Kitwe General Trader, CXC Africa, MMI Tanzania,
Mwandago Invesment Ltd, Break Point na GSM Media.
Vilevile uzinduzi huo utahamia
mkoa wa Arusha mara tu baada ya kufanyika mkoa wa Dar es Salaam.
Wasanii Linah Sanga anayeimba nyimbo za kizazi kipya na Wanne Star
msanii wa ngoma za asili watatoa burudani katika uzinduzi huo.
Mashindano ya Miss Tanzania
yalifungiwa kwa miaka miwili mfululizo na Baraza la Sanaa Tanzania
(BASATA) Desemba 22, 2014 kutokana na kukiuka Sheria, Kanuni na Taratibu
za uendeshaji matukio ya Sanaa nchini, kutokuwasilisha nyaraka
mbalimbali za shindano lake hususan mikataba ya washiriki pamoja na
kutumia mawakala wasiosajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.
Mashindano hayo yamefunguliwa
BASATA Agosti, 2015 baada ya mwandaaji wake LINO International Agency
Limited kufuata taratibu ikiwemo kuomba radhi na kuyafanyia kazi baadhi
ya mapungufu yaliyojitokeza pamoja na kutekeleza masharti aliyopewa.
Tags
KIBURUDANI